Raha kwa Lions Eye Hospital FC kupata pointi tatu
Na JOHN KIMWERE
TIMU ya Lions Eye Hospital FC ilitolewa kijasho chembamba kabla ya kuvuna ufanisi wa magoli 3-2 dhidi ya AFC Leopards Youth kwenye mechi ya Kanda ‘B’ kufukuzia taji la Nairobi West Regional League (RWRL) iliyosakatiwa Uwanjani Kabete Technical, Nairobi.
Lions ya kocha George Riziki ilijitahidi kiume kusaka alama tatu muhimu ambapo ilikutanishwa na ushindani mkali mbele ya wageni wao wanaonolewa na Boniface Ambani mchezaji wa zamani wa Yanga FC ya Tanzania.
Kwenye mchezo huo kila upande ulionyesha dalili za kufanya vizuri lakini pia kukaribia kutoshana nguvu. Lions Eye Hospital inayoshiriki kipute hicho kwa mara ya kwanza ilijiweka kifua mbele kupitia juhudi zake Sammy Ludias kabla Augustine Oduor kusawazishia AFC Leopards Youth dakika tano baadaye.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Lions Eye ikiongeza bao la lililofumwa kimiani na Sammy Ludias hata hivyo dakika tatu baadaye kwa mara nyingine, Augustine Oduor alisawazishia AFC Leopards Youth.
Wachana nyavu wa pande zote waliendelea kuonyesha ujuzi wao wakisaka kuongezea angalau bao la ushindi. Baada ya gonga gonga Richard Kairo alionyesha ubabe wake alipopenya na ngozi ya ng’ombe kunako dakika ya 85 na kutingia Lions Eye Hospital bao la tatu la ushindi.
Matokeo hayo yaliipiga jeki Lions Eye Hospital FC inayouguza majeraha ya kupokonywa pointi sita kwa madai ya kumchezesha mchezaji asiyefaa kwenye mechi zake mbili dhidi ya KEMRI FC na South B Allstars. Kitendo hicho kilifanya aliyekuwa kocha wake, Robert Orangi kupigwa kalamu.
Kwenye matokeo ya mengine kipute hicho, David Vusala alipiga kombora moja safi na kubeba KYSA Karangata kuchabanga KEMRI bao 1-0. KYSA Karangata ilinasa ufanisi huo wiki mbili baada ya kuandikisha sare ya bao 1-1 dhidi ya Lions Eye Hospitali FC. Nao wanasoka wa WYSA United walikung’uta South B Allstars magoli 3-2.
Kwenye mechi za Kundi A ngarambe hiyo, Collins Ochieng na Ikutwa Ford walicheka na nyavu mara moja kila mmoja na kusaidia Riruta United Makarios 111 FC kulaza viongozi Nairobi Prisons mabao 2-1. Nayo Waterworks iliinyamazisha Kibera Saints mabao 2-0 yaliyotingwa na Oscar Wamalwa na Daniel Ochieng huku Kibera Lexus ikinasa sare tasa dhidi ya Al Swafaa FC.