Michezo

RAHA TELE! Hatimaye Arsenal na Arteta waonja raha ya kushinda nyumbani

January 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

ARSENAL ilipatia mashabiki wake raha tele, ilipomaliza ukame wa karibu miezi mitatu bila ushindi uwanjani Emirates kwa kupiga mahasimu wa tangu jadi Manchester United 2-0, kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) Jumatano usiku.

Ushindi huo wa kwanza wa kocha mpya Mikel Arteta, na wa kwanza katika mechi 16 zilizopita, ulipatikana kupitia mabao ya Nicolas Pepe na Sokratis Papastathopoulos katika kipindi cha kwanza.

Arsenal ilianza mchuano huo wa raundi ya 21 ikiwa alama 12 nje ya mduara wa klabu nne za kwanza kufuzu kwa kombe la UEFA, na pointi nne tu juu ya maeneo hatari ya kutemwa nje ya ligi.

Hata hivyo, baada ya ushindi huo wa kwanza nyumbani katika siku 87, vijana wa Arteta wanafunga mduara wa 10-bora kwenye ligi hii ya klabu 20 kwa alama 27, nne nyuma ya nambari tano United.

Waliruka Everton, Southampton na Newcastle na sasa wako alama moja nyuma ya nambari tisa Crystal Palace, ambao watakutana nao katika mechi ijayo mnamo Januari 11.

“Nimefurahishwa sana na mchezo wetu. Nimefurahia matokeo hata zaidi,” alisema Arteta baada ya mechi hiyo yake ya tatu. “Kila kitu nilitaka kuona uwanjani, niliona leo usiku (Jumatano).”

Arsenal, ambayo ilizaba United 2-0 uwanjani Emirates msimu uliopita, ilikuwa imeonyesha dalili za kuamka ilipochuana mechi ya kwanza ya Arteta nyumbani Emirates, dhidi ya Chelsea mnamo Desemba 29.

Hata hivyo, ilitupa uongozi dakika za lala-salama na kupoteza 2-1.

Lakini Jumatano, Arsenal ilizidia United ujanja katika mechi ambayo imeibua maswali kuhusu uwezo wa vijana wa Ole Gunnar Solskjaer kukamilisha msimu ndani ya mduara wa timu nne-bora.

“Kwa wakati huu bado tunang’ang’ana kudumisha nguvu zetu mchezoni katika dakika zote tisini. Tutafaulu kudhibiti ulegevu huo. Lakini zaidi nilipendezwa na ari waliyoonyesha. Nilifurahia kuona wakijituma pamoja,” aliongeza Arteta.

Pogba nje

Vijana wa Solskjaer walimkosa tena kiungo Paul Pogba, ambaye anatarajiwa kuendelea kuwa mkekeni kwa mwezi mwingine baada ya kufanyiwa upasuaji wa kifundo, ambacho kimemweka nje kwa kipindi kikubwa msimu huu.

Kukosekana kwa Pogba bado kunaonekana kutatiza United kuunda nafasi za mashambulizi, na ilishindwa kujikwamua baada ya kufungwa bao la mapema.

“(Arsenal) Walikuwa wazuri kutuliko. Walionyesha ari, walipigania kila mpira waliopoteza na ilikuwa vigumu sana kupata mpira kutoka kwao,” alisema Solskjaer.