Rai ajiondoa kwa mbio za magari duru ya Kajiado
Na GEOFFREY ANENE
BINGWA mara tatu wa duru ya Nakuru ya Mbio za Magari za Kitaifa, Onkar Rai amefichua hatashiriki duru ya pili itakayofanyika katika kaunti ya Kajiado mapema mwezi Machi 2019.
Onkar ameeleza Shirikisho la Mbio za Magari za Kenya (KMSF) kwamba amekabwa na majukumu ambayo hawezi kuyaepuka.
“Nilikuwa nimetenga siku hiyo kwa shughuli fulani kwa hivyo sitaweza kushiriki duru ya pili. Kutegemea jinsi mambo yatakavyoenda, mimi na mwelekezi wangu tutarejea kutafuta taji katika duru ya tatu,” alisema Onkar, ambaye hajawahi kuibuka bingwa wa Kenya katika ligi hii ya duru nane.
Hata hivyo, mshindi huyu wa ligi ya daraja ya pili ameahidi kurejelea kampeni za kutafuta taji lake la kwanza kabisa la Kenya katika duru ya tatu itakayoandaliwa mjini Eldoret.
Onkar alinyakua taji la Nakuru Rally baada ya kulemea bingwa wa Kenya Carl “Flash” Tundo kwa sekunde nne pekee. Duru hiyo ilifanyika katika kaunti za Baringo na Nakuru katika maeneo ya Mogotio na Gicheha.
Onkar anaongoza msimu kwa alama 25 akifuatiwa na bingwa mtetezi Tundo (21), Baldev Chager (18) na kakake Onkar, Tejveer Rai (15).