Michezo

Rais Kenyatta atarajiwa kufungua uwanja wa Kinoru Julai 15

June 27th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

UWANJA wa Moi Kinoru katika Kaunti ya Meru utafunguliwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta baada ya shughuli za ukarabati kukamilika kufikia Julai 15, 2020.

Uwanja huo ulifungwa kwa kipindi cha miaka sita iliyopita ili kupisha mchakato wa ukarabati ambao unakisiwa kugharimu zaidi ya Sh1 bilioni.

Shughuli za kuupa uwanja huo sura mpya zilianza rasmi mnamo 2014 baada ya Serikali ya Kaunti ya Meru kutengea shughuli hizo jumla ya Sh200 milioni Kenya ilipoaminiwa fursa ya kuwa mwenyeji wa fainali za CHAN 2018.

Serikali Kuu ya Kitaifa ilichangia Sh892 milioni kwa minajili ya awamu ya pili ya shughuli za ukarabati wa uwanja wa Kinoru.

Japo kivumbi hicho cha CHAN kilitarajiwa kufanyika humu nchini, mwendo wa kobe katika ukarabati wa viwanja vya Kinoru, Nyayo jijini Nairobi, Kaunti ya Narok, Moi Kisumu na Kericho Green, ulichangia Kenya kupokonywa haki za kuwa mwenyeji wa kipute hicho kilichohamishiwa baadaye nchini Morocco mnamo Januari 12 – Februari 4, 2018.

Kufikia mwisho wa 2018, asilimia 65 ya kazi za ukarabati zilikuwa zimekamilika katika uwanja wa Kinoru. Gavana wa Kaunti ya Meru, Kiraitu Murungi ambaye ameukagua uwanja huo akiwa na Waziri wa Michezo, Amina Mohamed, amethibitisha kwamba mwanakandarasi aliyekuwa akishughulikia ukarabati wa uga huo tayari amepokezwa malipo yake yote na anatarajiwa kukabidhi uwanja kwa Serikali ya Kaunti kufikia Julai 15, 2020.

Mbali na vyumba viwili vya marefa, miongoni mwa vyumba vipya ambavyo pia vimejengwa kwa sasa katika uwanja wa Kinoru ni viwili vitakavyotumiwa kuwafanyia wanariadha vipimo vya kubaini iwapo wametumia dawa za kusisimua misuli na vinne vya wanamichezo kubadilishia sare.

Kumbi za mazoezi na michezo mbalimbali katika uwanja huo ulio na uwezo wa kubeba mashabiki 20,000 walioketi sasa zitakuwa pia na sura mpya baada ya kufanyiwa ukarabati.

Sehemu za kuchezea soka, hoki, voliboli, mpira wa vikapu na netiboli ambazo zimekuwa katika hali mbaya, pia zimekarabatiwa na kuwekewa mazulia mapya ya kisasa.