Michezo

Rangers roho juu ikikabili Stima ikitumai kuingia KPL

June 18th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN ASHIHUNDU

BINGWA wa mchujo wa kuwania nafasi ya kujiunga na Ligi Kuu ya Kenya (KPL) atapatikana kesho Jumatano baada ya mechi ya marudiano kati ya Posta Rangers na Nairobi Stima ugani Kenyatta Stadium, Machakos.

Tayari Rangers wametia guu moja KPL baada ya ushindi wao wa 2-1 dhidi ya wapinzani wao katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyochezewa Naivasha, mwishoni mwa wiki.

Kwenye mechi hiyo iliyochezewa uwanja wa Karuturi, Rangers walipata mabao yao dakika za tano na 58 kupitia kwa aliyekuwa mlinzi wa Harambee Stars Jockins Atudo na Francis Nambute.

Bao la Stima lilifungwa na mfungaji wa mabao mengi msimu huu kwenye ligi ya Supa Ligi (NSL), Dennis Ochieng Oalo.

Hii ni mara ya pili timu mbili kukutana kuwania nafasi ya kufuzu kwa ligi kuu, baada ya hapo awali Thika United kuvaana na Ushuru FC ambapo Thika walifanikiwa kufuatia ushindi wa jumla wa 2-1.

Mwishoni mwa wiki, vijana wa Stima walipungukiwa na makali baada ya kufungwa bao la pili, lakini wameahidi kurejea kwa kishindo timu hizo zitakapokutana kesho mjini Machakos.

“Tulipoteza mkondo wa kwanza kwa timu ambayo ina mastaa wengi walio na uzoefu wa mechi kubwa, lakini hatujakata tamaa,” alisema Oalo aliyewafungia bao la pekee.

“Tulicheza vizuri katika kipindi cha kwanza lakini tukapunguza makali mechi ilipokuwa ikielekea ukingoni. Tungali na matumaini ya kufuzu kwa Ligi Kuu,” aliongeza.

Mwenzake, John Kamau wa Rangers alisema: “Tuliingia uwanjani tukifahamu umuhimu wa mechi kama hiyo na tumejiandaa kucheza vizuri zaidi katika mechi ya marudiano kwa lengo la kufuzu na kushiriki Ligi Kuu msimu ujao.”

Timu itakayoshindwa kesho itacheza ligi ya NSL.

Rangers walimaliza KPL katika nafasi ya 16 kati ya timu 18, huku Stima wakimaliza NSL katika nafasi ya tatu nyuma ya Kisumu All Stars na Wazito FC ambazo zilifuzu moja kwa moja kuingia KPL.

Stima walishindwa mara mbili pekee kutokana na mechi 38 za NSL, na walimaliza ligi kwa pointi 80, sawa na Kisumu All Stars, lakini uchache wa mabao ulivuruga juhudi zao.

Vikosi

Rangers: Gradus Ochieng, Simon Mbugi, Collins Omondi, Charles Odete, Jockins Atudo, Joseph Mbugi, Gerson Likonoh, Peter Nganga, Marsellus Ingotsi, Francis Nambute na Felix Olouch.

Wachezaji wa akiba: Eluid Emase, Ezekiel Nyati, Jerry Santo, Elvis Osok, Joseph Nyaga, Jared Obwoge na Ken Mutembei.

Stima: Jacob Osano, Brian Odhiambo, Levian Ochieng, Shela Mandela, Joseph Shikokoti, Alex Luganji, Hillary Ojwang, Brian Musa, Patrick Asiku, Raphael Asudi na Dennis Oalo.

Wachezaji wa akiba: Muhammad Kasule, Shadrack Onyango, Joseph Njoroge, Benjamin Chaka, Erick Kinuthia, Paul Kisige na Daglas Mokaya.