Michezo

Rangers walaza Galatasaray na kutinga hatua ya makundi ya Europa League

October 3rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

RANGERS walitinga hatua ya makundi ya Europa League kwa msimu wa tatu mfululizo baada ya kuwapiga Galatasaray 2-1 mjini Ibrox, Scotland mnamo Oktoba 1, 2020.

Scott Arfield aliwaweka Rangers kifua mbele kunako dakika ya 52 baada ya kupokezwa krosi safi na Ianis Hagi huku James Tavernier akifanya mambo kuwa 2-0 dakika tisa baadaye.

Ingawa Galatasaray ya Uturuki wakifanya mashambulizi mengi langoni pa Rangers, walishindwa kutumia fursa za wazi walizozipata. Ilikuwa hadi mwishoni mwa kipindi cha pili ambao Galatasaray walifungiwa na beki Teixeira Marcao.

Kutokana na ushindi huo, Rangers walitiwa kwenye tapo la tatu katika droo ya hatua ya makundi iliyofanywa Oktoba 2, 2020.

Ufanisi wa Rangers chini ya kocha Steven Gerrard uliendeleza rekodi nzuri ya kutoshindwa kwa kikosi hicho katika jumla ya mechi 11 zilizopita kwenye mashindano yote. Rangers hawajashindwa pia katika mechi yoyote kati ya 19 zilizopita za kufuzu kwa Europa League chini ya ukufunzi wa Gerrard ambaye ni raia wa Uingereza.

Galatasaray waliondoka uwanjani wakilalamikia maamuzi ya refa Andris Treimanis kuwanyima mkwaju wa penalti baada ya kuhisi kwamba mpira uliopigwa na kiungo Sofiane Feghouli uligusa mkono wa Connor Goldson ndani ya kijisanduku cha Rangers.

Galatasaray waliokamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uturuki katika nafasi ya sita mnamo 2019-20 walimiliki asilimia kubwa ya mpira na waliowazidi wenyeji wao maarifa kwa kipindi kirefu.

Rangers kwa sasa wanajiandaa kuwa wageni wa Ross County katika Ligi Kuu ya Scotland mnamo Oktoba 4, 2020.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO