Rangers wapaa Gor Mahia wakisalia kileleni mwa KPL
Na GEOFFREY ANENE
POSTA Rangers ndiyo timu iliyoimarika zaidi kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Kenya (KPL) baada ya kulipua washiriki wapya Kisumu All Stars 3-0 ugani Machakos katika mechi ya raundi ya tano Jumatatu na kuruka juu nafasi saba hadi nambari tano.
Mabingwa watetezi Gor Mahia wanasalia kileleni kwa alama 12 baada ya kuandikisha ushindi wa nne mfululizo walipokung’uta Zoo 1-0 Jumapili.
Wanabenki wa KCB na wanamvinyo Tusker wako juu katika nafasi ya tatu na tano baada ya kulima Nzoia Sugar 1-0 na Kakamega Homeboyz 3-1, mtawalia.
KCB sasa inashikilia nafasi ya pili kwa alama 10 ikizidia Tusker ubora wa magoli.
Western Stima, ambayo ilikabwa 0-0 na wanajeshi wa Ulinzi Stars, imepisha KCB na Tusker na kutulia katika nafasi ya tatu kwa alama tisa.
Rangers, ambayo haikuwa imepata ushindi katika mechi tatu, imekalia nafasi ya tano kwa alama nane, sawa na Ulinzi na Bandari zinazofuatana katika nafasi ya sita na saba mtawalia. Bandari ilizabwa 2-1 na Sofapaka mnamo Jumapili.
AFC Leopards, ambayo haikuwa na mechi wikendi, imeteremka kutoka nafasi ya tatu hadi nambari nane.
Klabu hiyo maarufu kama ‘Ingwe’ ina alama saba.
Inatofautiana na Sofapaka, Homeboyz na Mathare United kwa ubora wa magoli tu.
Sofapaka yasalia katika nafasi ya tisa
Sofapaka ilisalia katika nafasi ya tisa nayo Homeboyz imetupwa chini kutoka nafasi ya nne hadi nambari 10.
Mathare ilikwamilia nafasi ya 11 ikifuatiwa na Wazito iliyoshuka nafasi mbili. Mathare na Wazito zilitoka 2-2 wikendi.
Wazito ina alama sita sawa na nambari 13 Kariobangi Sharks iliyoandikisha ushindi wake wa kwanza msimu huu ilipobwaga Chemelil Sugar 2-0 na kuruka Nzoia Sugar. Nzoia ina alama nne.
Hakuna mabadiliko katika nafasi nne za mwisho zinazoshikiliwa na Zoo na SoNy (alama tatu), Kisumu (alama moja) nayo Chemelil inavuta mkia bila alama.