Michezo

Rashford aongoza Manchester United kupepeta PSG kwa mara nyingine katika UEFA

October 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

CHIPUKIZI Marcus Rashford alisaidia Manchester United kuendeleza ubabe wao dhidi ya Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa kwenye gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Hii ni baada ya Man-United kuwapepeta wanafainali hao wa 2019-20 kwa mabao 2-1 mnamo Oktoba 20 ugani Parc des Princes, Ufaransa.

Hiyo ilikuwa mara ya kwanza tangu Disemba 2004 walipopigwa 3-1 na CSKA Moscow kwa PSG kupoteza mechi ya makundi ya UEFA katika uwanja wao wa nyumbani.

Bruno Fernandes aliwaweka Man-United kifua mbele kupitia penalti ya dakika ya 23 kabla ya PSG kusawazisha kupitia Anthony Martial aliyejifunga dakika 10 baada ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa kipindi cha pili kupulizwa. Rashford alifungia waajiri wake, ambao kwa sasa wamejifunga mara tisa kwenye UEFA, bao la ushindi kunako dakika ya 87.

Penalti ya dakika za mwisho kutoka kwa Rashford ugani Parc des Princes miezi 18 iliyopita ilishuhudia Man-United wakitoka chini kwa mabao 2-0 katika mkondo wa kwanza na kuwabandua PSG kwa kanuni ya wingi wa mabao ya ugenini baada ya kusajili ushindi wa 3-1 katika mkondo wa pili jijini Paris.

PSG kwa sasa wana ulazima wa kusajili ushindi kwenye mechi yao ijayo dhidi ya Istanbul Basaksehir waliopigwa 2-0 na RB Leipzig katika gozi jingine la Kundi H Oktoba 20.

Tangu mwanzo wa msimu jana wa 2019-20, Man-United wamepokezwa jumla ya penalti 27 ambayo zimewapa mabao 22 dhidi ya wapinzani wao kwenye Ligi Kuu tano za bara Ulaya nchini Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia na Uhispania.

Fernandes aliyesajiliwa na Man-United mnamo Januari 2019, amehusika kwenye mabao 27 ya kikosi hicho baada ya kufunga magoli 16 na kuchangia mengine 11.

Mechi kati ya PSG na Man-United mnamo Jumanne ilishuhidia fowadi Neymar Jr akishindwa kufungia waajiri wake kwa mara ya nne mfululizo kwenye UEFA tangu Novemba 2013.