Rashford atuzwa na Malkia wa Uingereza
Na MASHIRIKA
FOWADI wa Manchester United, Marcus Rashford ametawazwa Mwanachama wa Dola la Uingereza almaarufu Member of the Order of the British Empire (MBE) na ametiwa kwenye orodha ya waheshimiwa watakaokuwa wakihudhuria maadhimisho ya siku ya kuzaliwa kwa Malkia wa Uingereza.
Rashford, 22, alipigia serikali ya Uingereza kampeni za kuruhusu takriban watoto 1.3 milioni kupata chakula cha bure wakati shule zilipofungwa ghafla mapema mwaka huu wa 2020 kutokana na janga la corona.
Sogora huyo alimtaka pia Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson kurefusha kipindi cha kutolewa kwa msaada huo wa chakula kwa wanafunzi.
Mwanzilishi wa mbio za Great North Run, Brendan Foster pia ametawazwa na Malkia wa Uingereza.
Mwanariadha huyo aliyeibuka bingwa wa mbio za mita 10,000 kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola, aliwahi pia kuwakilisha Uingereza katika makala matatu ya Michezo ya Olimpiki kabla ya kujitosa katika ulingo wa utangazaji wa michezo mnamo 1980.
Mbio alizoziasisi za Great North Run ni miongoni mwa matukio makubwa zaidi ambayo huvutia idadi kubwa ya mashabiki katika ulingo wa riadha nchini Uingereza.
Hadi alipostaafu kwenye utangazaji mnamo 2017, Foster alikuwa ametangaza makala tisa ya Michezo ya Olimpiki.
Katika ulingo wa raga, waliotambuliwa na kutuzwa na Malkia wa Uingereza ni kocha mkuu wa timu ya taifa ya Wales, Warren Gatland na mkufunzi wa zamani wa kikosi hicho, Gareth Thomas. Wawili hao wametawazwa kuwa Commander of the Most Excellent Order of the British Empire (CBE).
Alun Wyn Jones ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya raga ya Wales, ametawazwa Officer of the Most Excellent Order of the British Empire (OBE).
Bingwa mara tatu wa Olimpiki katika fani ya kutunisha misuli Eve Muirhead kutoka Scotland ametawazwa Member of the Order of the British Empire (MBE) kwa pamoja na bingwa mara 12 wa Olimpiki katika mchezo wa kucheza ni mipira mezani (snooker), Reanne Evans na mwanakriketi wa zamani wa Uingereza, Darren Gough.
Orodha ya wanamichezo waliotarajiwa kutuzwa na Malkia ilikuwa mwanzo itolewe Juni 2020 kabla ya shughuli hiyo kuahirishwa kwa sabau ya janga la corona.