Michezo

Ratiba za Riadha za Dunia na Jumuiya ya Madola zagongana

April 11th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Riadha la Kenya (AK) litalazimika kuunga vikosi tofauti kwa minajili ya kushiriki fani mbalimbali katika makala yajayo ya Riadha za Dunia na Jumuiya ya Madola.

Hii ni baada ya Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) kuthibitisha kwamba mashindano hayo mawili ya haiba kubwa yataandaliwa kwa takriban kipindi kimoja mnamo 2022.

Kwa mujibu wa ratiba mpya iliyotolewa jana na IAAF, Riadha za Dunia sasa zitaandaliwa kati ya Julai 15-24, 2021 jijini Oregon, Amerika. Awali, maandalizi kwa ajili ya mashindano hayo yaliyokuwa yafanyike mapema mwaka ujao, yaliahirishwa kwa hofu ya kusambaa zaidi kwa maambukizi ya virusi vya corona.

Aidha, makala ya 22 ya Michezo ya Jumuiya ya Madola yatasalia kufanyika kati ya Julai 27 hadi Agosti 7 jijini Birmingham, Uingereza jinsi yalivyoratibiwa hapo awali.

Kuratibiwa upya kwa Riadha za Dunia za 2021 kulichochewa na hatua ya kuahirishwa kwa Olimpiki zilizokuwa zifanyike jijini Tokyo, Japan kati ya Julai 24 na Agosti 9, 2020. Michezo ambayo huandaliwa kila baada ya miaka minne sasa itafanyika kati ya Julai 23 na Agosti 8, 2021.

Kwa mujibu wa Bernard Ouma ambaye ni kocha maarufu wa riadha humu nchini, kuandaliwa kwa Riadha za Dunia na Michezo ya Jumuiya ya Madola kwa wakati mmoja unaokaribiana sana, kutawaathiri sana watimkaji wa mbio za masafa marefu na yale ya kadri.

Kwa upande wake, Julius Yego aliyeibuka bingwa wa dunia katika fani ya urushaji mkuki mnamo 2015, amedokeza uwezekano wa ladha ya Michezo ya Jumuiya ya Madola kuyeyushwa zaidi kwa sababu wanariadha wengi watapania kunogesha Riadha za Dunia iwapo wataruhusiwa kuchagua michezo ya kushiriki kwa hiari yao. Yego aliibuka mfalme wa urushaji mkuki katika Michezo ya Jumuiya ya Madola mnamo 2014.

Faith Chepng’etich aliyeibuka mshindi wa nishani ya dhahabu katika mbio za mita 1,500 kwenye Olimpiki za 2016 jijini Rio, Brazil, amesema kwamba itawawia vigumu wanariadha kushiriki Riadha za Dunia na Jumuiya ya Madola kwa pamoja bila ya fomu na afya yao kuathirika.

Chepng’etich alijitwalia pia medali ya dhahabu katika mbio za mita 1,500 kwenye Riadha za Dunia za London, Uingereza mnamo 2017 kabla ya kuambulia nishani ya fedha jijini Doha, Qatar mnamo 2019.

Kauli ya Chepng’etich ilishadidiwa na bingwa wa dunia na Jumuiya ya Madola katika mita 5,000, Hellen Obiri aliyehifadhi taji lake katika mbio hizo jijini Doha mwaka jana.

“Zaidi ya Riadha za Dunia na Jumuiya ya Madola, pia kuna Olimpiki, kivumbi cha Diamond League na michezo ya World Continental Tour. Itahitaji mwanariadha mweledi zaidi kushiriki mbio hizi zote na atambe. Kushiriki hata mbili kati ya mbio hizi kwa kipindi kimoja pia ni hatari sana,” akasema Obiri aliyeambulia nishani ya fedha katika mbio za mita 5,000 kwenye Olimpiki za 2016 jijini Rio.