Michezo

RB Leipzig yapiga Atletico Madrid na kufululiza hadi nusu-fainali za UEFA kuvaana na PSG

August 14th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha RB Leipzig kiliwabandua Atletico Madrid kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa mabao 2-1 jijini Lisbon, Ureno mnamo Agosti 13, 2020.

Mafanikio hao ya Leipzig kutoka Ujerumani uliwakatia tiketi ya kushiriki nusu-fainali za UEFA kwa mara ya kwanza tangu klabu hiyo ianzishwe miaka 11 iliyopita.

Baada ya mwanzo mbaya kwenye kipindi cha kwanza, Dani Olmo aliwaweka Leipzig kifua mbele kunako dakika 50 kabla ya Joao Felix kusawazisha mambo kupitia penalti ya dakika ya 71.

Bao la Olmo lilimfanya kuwa Mhispania kwa kwanza kuwahi kufunga goli dhidi ya Atletico katika gozi la UEFA tangu Miguel Marcos Madera afanye hivyo walipokutana na FK Qarabag ya Azerbaijan mnamo Oktoba 2017.

 

Kiungo wa RB Leipzig Mhispania Dani Olmo (kushoto) apambana kudhibiti mpira dhidi ya Kiungo wa Atletico Koke katika robo-fainali ya UEFA Champions League uwanjani Jose Alvalade jijini Lisbon Agosti 13, 2020. Picha/ AFP

Atletico waliokuwa wakiwania fursa ya kutinga fainali ya UEFA kwa mara ya tatu baada ya miaka sita, walionekana kuridhika na sare katika mchuano huo wa mkondo mmoja huku dalili zote zikiashiria kwamba walitaka mechi iende hadi muda wa ziada na ikiwezekana mshindi aamuliwe kupitia mikwaju ya penalti.

Badala ya kushambulia, Atletico sasa waliibana ngome yao na kila mchezaji akawa mlinzi.

Hata hivyo, hatua hiyo yao iliwaweka katika presha zaidi kutoka kwa wavamizi wa Leipzig waliowashambulia kila dakika na kuonekana kuwalemea wapinzani wao katika takriban kila idara.

Ilikuwa hadi dakika ya 88 ambapo Tyler Adams aliwafungia Leipzig bao la pili na kusaidia kikosi hicho cha kocha Julian Naglesmann kujikatika tiketi ya kumenyana na Paris Saint-Germain (PSG) kwenye hatua ya nne-bora.

Leipzig walijibwaga uwanjani kwa minajili ya mechi hiyo bila huduma za mshambuliaji wao matata, Timo Werner aliyekamilisha uhamisho wake hadi Chelsea kwa Sh7.5 bilioni.

Hadi kuondoka kwake kambini mwa Leipzig, Werner alikuwa amefungia kikosi hicho jumla ya mabao 34 kutokana na mapambano yote ya msimu huu.

Leipzig inakuwa kikosi cha kwanza kutoka Ujerumani baada ya Bayern Munich na Borussia Dortmund kutinga nusu-fainali ya UEFA tangu Schalke wafanye hivyo mnamo 2010-11.

Atletico wameshindwa kusonga mbele kwenye UEFA dhidi ya mpinzani kutoka Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kwa mara ya kwanza katika hatua ya mwondoano. Awali, walikuwa wamefaulu kuwaangusha Bayer Leverkusen mara mbili na Bayern Munich mara moja.