Real Madrid wala sare ya Sociedad
Na MASHIRIKA
MABINGWA watetezi Real Madrid walikabwa koo na kulazimishiwa sare tasa na Real Sociedad katika mchuano wa kwanza wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu huu.
Kikosi hicho cha kocha Zinedine Zidane kilianza kampeni zake wiki moja baada ya timu nyinginezo kwa kuwa kilishiriki soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mwezi uliopita.
Ingawa hivyo, walikosa kuridhisha matarajio ya mashabiki dhidi ya Sociedad na wakapata fursa chache sana za kufunga mabao. Jaribio la kwanza la Real langoni pa wenyeji wao lilikuwa katika dakika ya 24 ila kombora lake likapanguliwa kirahisi na kipa Alex Remiro.
Mchuano huo ulikuwa wa kwanza kiungo na nahodha wa zamani wa Manchester City, David Silva, kushiriki tangu aingie katika sajili rasmi ya Sociedad.
Sociedad nao walipata nafasi nyingi za wazi ila wakazipoteza. Alexander Isak alisalia uso kwa uso na kipa Thibaut Courtois katika dakika ya 28, sekunde chache baada ya Ander Barrenetxea kupaisha mpira ambao vinginevyo ungewaweka waajiri wake kifua mbele.
Real walikosa huduma za kiungo Eden Hazard anayeuguza jeraha la kifundo cha mguu kwenye mechi hiyo.
Kuondoka kwa Gareth Bale aliyeyoyomea Tottenham Hotspur kwa mkopo kulitoa nafasi kwa washambuliaji chipukizi wazawa wa Brazil, Vinicius Junior na Rodrygo kushirikiana na Benzema katika safu ya mbele ya Real huku Martin Odegaard akitegemewa pakubwa katika safu ya kati.
Fataki kali za Dani Carvajal zilipanguliwa pia kirahisi na kipa Remiro aliyefanya kazi ya ziada na kumzima Toni Kroos wa Real waliomwajibisha kiungo Marvin Park nafasi ya kucheza katika kipindi cha pili. Park alisajiliwa na Real mwanzoni ma msimu huu baada ya kuchezea Tranmere Rovers kwa kipindi cha miaka mitatu.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO