Michezo

Real Madrid washinda kwa mara ya kwanza baada ya michuano minne ligini

December 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

REAL Madrid walikomesha rekodi ya kutoshinda mechi yoyote kati ya tatu za awali kwa kujinyanyua dhidi ya Sevilla mnamo Disemba 5, 2020 na kuwapokeza kichapo cha 1-0 kwenye Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Bao la pekee na la ushindi kwa upande wa Real lilifumwa wavuni na kipa Yassine Bounou wa Sevilla aliyejifunga baada ya kushindwa kudhibiti kombora aliloelekezewa na fowadi Vinicius Jr.

Sevilla walionekana kuzidiwa maarifa katika kila idara kwenye mchuano huo huku wakielekeza mikwaju mitatu pekee kwenye lango la wageni wao. Mbali na Luuk de Jong, wengine waliojaribu kumtatiza kipa Thibaut Courtois ni Lucas Ocampos na Suso.

Karim Benzema alipoteza nafasi nyingi za wazi za kufungia Real ambao ni mabingwa watetezi wa La Liga huku ushirikiano kati yake na kiungo Toni Kroos ukishindwa kuzaa matunda yoyote.

Ushindi huo wa Real ambao wanatiwa makali na kocha Zinedine Zidane uliwapaisha hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali kwa alama 20, nne nyuma ya nambari mbili Real Sociedad. Atletico Madrid ya kocha Diego Simeone inaselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 26 licha ya kwamba ina mchuano mmoja zaidi wa kusakata kufikia idadi ya mechi ambazo zimepigwa na Real, Sociedad na nambari nne Villarreal.

Ushindi wa Real dhidi ya Sevilla ambao ni mabingwa wa Europa League unatarajiwa kuwapa motisha zaidi ya kupepeta Borussia Monchengladbach ya Ujerumani ambayo itavaana nao mnamo Disemba 9, 2020 kwenye mchuano wa mwisho wa makundi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Iwapo Real watazidiwa ujanja na M’gladbach kwenye mechi hiyo itakayochezewa uwanjani Afredo di Stefano, basi masogora wa Zidane ambao ni mabingwa mara 13 wa taji la UEFA, watabanduliwa kwenye kampeni za kipute hicho msimu huu katika hatua ya makundi.