Real Madrid yagaragaza Barca katika El Clasico
Na MASHIRIKA
MADRID, Uhispania
REAL Madrid waliwazaba mahasimu wao Barcelona magoli 2-0, katika gozi la El Clasico ugani Santiago Bernabeu, Jumapili usiku.
Ushindi huo ulipaisha Real hadi kileleni mwa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kwa alama 56, moja mbele ya Barcelona ambao ni mabingwa watetezi.
Nao Sevilla waliwapepeta Osasuna 3-2 na kuchupa hadi nafasi ya tatu kwa pointi 46. Wako alama moja mbele ya Getafe ambao kwa sasa wanafunga mduara wa nne-bora, baada ya kuwapokeza Mallorca kichapo cha 1-0.
Vinicius Junior aliweka Real kifua mbele dakika ya 71, baada ya kushirikiana vilivyo na kiungo wa kati, Isco aliyechangia pia bao la pili lilofumwa wavuni na Mariano Diaz Mejia mwisho wa kipindi cha pili.
Bao la Mariano lilikuwa lake la kwanza katika mchuano wake wa kwanza akivalia jezi ya Real msimu huu.
Chini ya kocha Zinedine Zidane msimu jana, Real walikamilisha kampeni za La Liga katika nafasi ya pili kwa alama 19, nyuma ya Barcelona waliotawazwa wafalme.
Ilivyo, dalili zote zinaashiria kwamba kinyang’anyiro cha muhula huu kitatawaliwa na ushindani mkali kati ya mahasimu hao wanaotenganishwa na alama moja pekee kileleni mwa jedwali.
Hadi waliposhuka dimbani kuvaana na Barcelona, Real walikuwa wameambulia sare mbili ligini. Aidha, walipokezwa kichapo cha 2-1 kutoka kwa Manchester City katika dimba la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).
Zaidi ya msukumo wa kujinyanyua baada ya matokeo hayo duni, Real walikuwa na ulazima wa kufuta rekodi mbovu dhidi ya Barcelona, ambao walikuwa wamewapiga mara tano na kusajili sare mbili katika El Clasico saba zilizopita.
Kwa upande wao, Barcelona, inayonolewa na kocha Quique Setien, ilijitosa ugani ikijivunia ushindi katika mechi nne mfululizo uwanjani Bernabeu.
Wakipania kuendeleza ubabe wao dhidi ya Real, Barcelona walianza kivumbi hicho kwa matao ya juu ila bahati ikakataa kusimama nao.
Nyota Antoine Griezmann, Lionel Messi, Jordi Alba na Arthur Mello nusura wapachike mabao ya mapema ila walinyimwa nafasi na kipa Thibaut Courtois wa Real.
Katika mkondo wa kwanza wa gozi hilo la El Clasico msimu huu, Barcelona na Real ziliambulia sare tasa uwanjani Camp Nou, mnamo Disemba 2019.
Hiyo ilikuwa mara ya kwanza tangu 2002 kwa kipute hicho kukamilika bila ya miamba hao wote wa soka ya Uhispania kufungana.
Kwa mujibu wa Zidane, udhaifu mkubwa wa kikosi chake umekuwa katika safu ya mbele ambayo imekuwa ikiongozwa na nyota Karim Benzema anayejivunia mabao 13 kutokana na michuano 26 iliyopita ligini.
Setien alikidumisha kikosi kilichowalazimishia Napoli sare ya 1-1 ugenini katika mechi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mwanzoni mwa wiki iliyopita.