• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 2:58 PM
Red Carpet FC: Ukata unavyodidimiza azimio lake

Red Carpet FC: Ukata unavyodidimiza azimio lake

Na JOHN KIMWERE

TIMU za michezo huanzishwa kwa malengo tofauti ikiwamo kupalilia vipaji vya wachezaji chipukizi ili wakomae na wafuzu kushiriki mashindano ya kimataifa. Pia hatuwezi kuweka katika kaburi la sahau kwamba wahenga waliloga kuwa ‘Samaki mkunje angali mbichi.’

Miongoni mwanzo ni Red Carpet inayopatikana eneo la Kangemi Kaunti ya Nairobi. Timu hiyo iliyoasisiwa na kocha, Meshack Osero Onchonga ni kati ya vikosi 22 vilivyoshiriki kampeni za Nairobi West Regional League (NWRL) msimu uliopita kabla ya mlipuko wa corona kutua nchini.

Red Carpet ambayo huchezea mechi zake katika Uwanja wa Kihumbu-ini ilizaliwa mwaka 2007. Kocha huyo anasema alianzisha kikosi hicho ili kunoa talanta za wachezaji wanaokuja.

PANDASHUKA

”Ingawa tunapitia changamoto kibao ikiwamo kukosa ufadhili tunaendelea kupiga tizi tunakojiandaa kupambana mwanzo mwisho kwenye kampeni za muhula ujao,” kocha huyo alisema na kuongeza kuwa wachana nyavu wake wanaouwezo wa kutenda kweli ila pandashuka za ufadhili hudidimiza juhudi zao katika mchezo huo.

Anasisitiza kwamba bado hajatimiza ndoto ya kuchomoa wachezaji kadhaa kuchezea timu ya harambee Stars.

”Kiukweli huwa ni fahari kuu kwa kocha yoyote akinoa wachezaji hatimaye kuteuliwa kuwakilisha taifa kwenye mashindano ya kimataifa. Hata hivyo sijavunjika moyo wala kuyeyusha tumaini la kutimiza azimio langu,” akasema.

UFADHILI

Anasema vijana wake wanatarajia kazi zito kwenye kampeni za kipute cha NWRL muhula ujao hasa mbele ya vikosi mahiri kama Nairobi Prisons kati ya zingine.

Anashikilia kuwa endapo watapata mdhamini ana imani tosha kwamba ndani ya misimu miwili hawatakuwa na kijisababu cha kutofanya vizuri na kutwaa tiketi ya kufuzu kushiriki soka la daraja la juu.

Kando na ufadhili ukosefu wa Uwanja ni tatizo lingine maana zaidi ya klabu 15 ndizo hutegemea Uwanja wa Kihumbu-ini ambapo kila moja hutumia saa moja kushiriki mazoezi.

SUPER CUP

Red Carpet inajumuisha wachezaji kama: Erick shivoga, Geofrey Alma na Francis Mmnai (nahodha na naibu wake), Godfrey Odongi, Jeff Owino, Richie Simanyi, John Kamau, Vitalis owiti, Timothy Murunga na Patrick Otiende kati ya wengine.

Klabu hiyo tangia ianzishwe inajivunia kunyanyua taji la Tim Wanyonyi Super Cup 2018 ilipolaza Leeds United mabao 4-2 kupitia mipigo ya matuta baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1. Kikosi hicho kilinasa taji hilo licha ya kulinyemelea kwa miaka kadhaa huku ikiweka tumaini kuwa baada ya dhiki ni faraja.

  • Tags

You can share this post!

Wakenya watatu wapinga kuvunjwa kwa Bunge

Young Elephant yapania kushiriki Elite League msimu ujao