Michezo

REDS MAVIZIONI: Liverpool wala tupa kukata Norwich EPL

August 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

LIGI Kuu ya Uingereza ya msimu wa 2019-2020 inang’oa nanga leo Ijumaa, huku mabingwa wa Bara Ulaya, Liverpool wakitarajiwa kutuma onyo kwa wapinzani wote, watakapoalika Norwich uwanjani Anfield.

Vijana wa kocha Jurgen Klopp watashuka katika uwanja huu wa nyumbani na asilimia kubwa ya kuzoa alama tatu katika msimu mwingine unaotarajiwa kusisimua kama uliopita.

Mabingwa wa Uingereza mara 18 Liverpool walikamilisha ligi katika nafasi ya pili msimu uliopita nao Norwich wamepanda ngazi baada ya kushinda Ligi ya Daraja ya Pili.

Liverpool, ambayo ilishinda Ligi Kuu mara ya mwisho msimu wa 1989-1990, inajivunia wachana-nyavu matata Mohamed Salah, Sadio Mane na Roberto Firmino. Wanatarajiwa kuwa miiba Norwich.

Mbali na kuwa na washambuliaji hao hodari, Liverpool imekuwa ikifungua msimu vizuri.

Kwa kipindi cha miaka sita, Liverpool imeandikisha ushindi mara tano na sare moja katika mechi yake ya kuanza msimu.

‘The Reds’ pia haijashindwa na timu inayoingia ama kurejea kwenye Ligi Kuu katika mechi 11 zilizopita. Vilevile, Liverpool haijashindwa katika mechi 25 zilizopita dhidi ya timu zilizopandishwa daraja.

Pia, inajivunia rekodi nzuri sana ya kutoshindwa na Norwich ikiwemo kuishinda mara nane na kutoka sare mechi mbili tangu milenia mpya.

Mara ya mwisho klabu hizi zilikutana ligini ilikuwa msimu 2015-2016 kabla Norwich itemwe.

Zilitoka 1-1 uwanjani Anfield kabla ya mabao tisa kushuhudiwa katika mechi ya marudiano ambayo Liverpool ilitawala 5-4.

Firmino alipachika mawili nao James Milner, Jordan Henderson na Adam Lallana walitikisa nyavu za Norwich iliyoona lango kupitia kwa Sebastien Bassong, Wesley Hoolahan, Dieumerci Mbokani na Steven Naismith. Wafungaji hao wote wa Liverpool bado wanaichezea nao Bassong, Hoolahan, Mbokani na Naismith si wachezaji wa Norwich.

Salah na Mane waliibuka wafungaji bora msimu uliopita kwa pamoja na Pierre-Emerick Aubameyang wa Arsenal kwa kucheka na nyavu mara 22 kila mmoja.

Mane ana rekodi nzuri katika siku ya kufungua msimu akifunga katika kila mechi ya kuanza msimu katika misimu mitatu iliyopita.

Hakutumiwa katika mechi ya Community Shield dhidi ya mabingwa Manchester City wikendi iliyopita akipewa likizo zaidi baada ya kufikisha Senegal katika fainali ya Kombe la Afrika (AFCON) nchini Misri.

Hali nzuri

Huenda Klopp akatumia Divock Origi badala ya Mane ili kupatia raia huyo wa Senegal muda zaidi kuwa katika hali nzuri.

Origi alifungia Liverpool mabao muhimu msimu uliopita, hasa katika Klabu Bingwa Ulaya. Anatarajiwa kushirikiana na mwanasoka bora wa Afrika mwaka 2017 na 2018 Salah pamoja na Firmino.

Beki matata Virgil van Dijk ataongoza ulinzi wa Liverpool katika mechi hii ambayo kiungo Milner huenda asicheze baada ya kupata jeraha ndogo dhidi ya City.

Mchuano huu utakuwa wa kwanza kabisa kwenye ligi zote kuu kwa kocha Daniel Farke ambaye atakosa huduma za Christoph Zimmermann, Alex Tettey na Louis Thompson.

Tegemeo hawa wamekuwa mkekani na majeraha. Hata hivyo, Norwich ina mshambuliaji matata Teemu Pukki kutoka Finland.

.