• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Refa wa mechi ya Gor dhidi ya Lobi Stars ya Nigeria atajwa

Refa wa mechi ya Gor dhidi ya Lobi Stars ya Nigeria atajwa

Na GEOFFREY ANENE

MAAFISA watakaosimamia mechi ya raundi ya kwanza ya Klabu Bingwa Afrika kati ya wenyeji Gor Mahia na wageni Lobi Stars kutoka Nigeria jijini Nairobi hapo Desemba 16, wametajwa.

Shirikisho la Soka la Bara Afrika (CAF) limetangaza kwamba Mtunisia Slim Belkhouas atakuwa refa wa kupuliza kipenga. Atasaidiwa na wanyanyuaji vibendera Khalil Hasaani na Jridi Faouzi pia kutoka Tunisia. Mtunisia Nasrallah Jaouadi atakuwa afisa wa nne. Mganda Mike Letti atahudumu kama kamishna wa mechi.

Mechi hii itasakatwa katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani unaobeba mashabiki 60, 000. Gor ilijikatia tiketi ya kushiriki raundi ya kwanza baada ya kubandua nje miamba wa Malawi, Nyasa Big Bullets kwa njia ya penalti 4-3 baada ya mikondo miwili ya awamu ya kuingia raundi ya kwanza kukamilika 1-1. Gor ilishinda 1-0 jijini Nairobi nayo Nyasa ikapata ushindi sawa na huo jijini Blantyre kabla ya mikwaju hiyo ya penalti kutumiwa kuamua timu itakayosonga mbele.

Lobi ililimwa 1-0 na UMS de Loum nchini Cameroon kabla ya kufuzu kushiriki raundi ya kwanza kwa kuchapa Wakamerun hao 2-0 katika mechi ya marudiano. Mshindi wa raundi ya kwanza ataingia mechi za makundi, huku atakayepoteza akateremka katika mashindano ya daraja ya pili ya Kombe la Mashirikisho. Kariobangi Sharks inawakilisha Kenya katika Kombe la Mashirikisho.

  • Tags

You can share this post!

Simiyu mwingi wa matumaini Shujaa itatamba licha ya matokeo...

Mahakama yampa idhini Timothy Njoya kumtimua ‘mama...

adminleo