Michezo

Rhonex, Tirop na Cheruiyot watwaa mataji Diamond League, Obiri na ndugu Manangoi wasikitisha

May 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

RHONEX Kipruto, Agnes Jebet Tirop na Timothy Cheruiyot waliibuka washindi wa mbio za mita 10,000, mita 5,000 na mita 1,500 kwenye duru ya tatu ya Riadha za Daimond League iliyoshuhudia malkia wa Dunia, Jumuiya ya Madola na Afrika wa mita 5,000 Hellen Obiri akiduwazwa jijini Stockholm nchini Uswidi, Alhamisi usiku.

Kipruto alibwaga wakimbiaji 26 katika mbio za mizunguko 25 alipozikamilisha kwa dakika 26:50.16. Alifuatwa kwa karibu na Muethiopia Hagos Gebrhiwet (27:01.02) na raia wa Eritrea Aron Kifle (27:27.68).

Wakenya Amos Kurgat, Charles Muneria, Peter Kiprotich na Vincent Rono walimaliza katika nafasi za saba, 12, 17 na 20 mtawalia, huku Gevin Kerich, Isaac Kipsang na Kelvin Kiptum wakikosa kukamilisha.

Tirop alifanya mambo katika mbio za mizunguko 12 na nusu alipotwaa taji kwa dakika 14:50.82 mbele ya Muethiopia Fantu Worku (14:51.31) na Mkenya mwingine Lilian Kasait (14:51.34).

Wakenya Caroline Chepkoech, Margaret Chelimo, Gloria Kite na Obiri walikamilisha katika nafasi za tano, sita, 10 na 12 mtawalia, huku Loice Chemnung na Mary Kuria wakiambulia pakavu.

Obiri alishinda mbio za kilomita 10 za Mbio za Nyika za Dunia mnamo Machi 30 nchini Denmark, mbio za mita 3,000 katika duru ya ufunguzi jijini Doha nchini Qatar mnamo Mei 3 na mbio za kilomita 10 za Simplyhealth Great Manchester Run nchini Uingereza mnamo Mei 19 kabla ya masikitiko ya Stockholm.

Cheruiyot alitamba katika mbio za mita 1,500 ambazo Wakenya wenzake Elijah Manangoi na George Manangoi, ambao ni ndugu, walikuwa wamepigiwa upatu.

Cheruiyot alitwaa taji kwa dakika 3:35.79 akifuatwa zaidi ya sekunde mbili nyuma na Ayanleh Souleiman kutoka Djibouti (3:37.30) na Jakob Ingebrigtsen wa Norway (3:37.30) mtawalia.

Matokeo ya kusikitisha

Wakenya Bethwel Birgen, Charles Simotwo, George Manangoi na Elijah Manangoi walimaliza katika nafasi ya nne, sita, nane na 10, mtawalia. Timothy Sein na Cornelius Tuwei hawakumaliza kitengo hiki cha mbio za mizunguko mitatu.

Mkenya wa pekee katika mbio za mita 800 za wanaume, Nicholas Kiplangat Kipkoech alisikitisha kwa kumaliza katika nafasi ya nane kati ya washiriki 10. Amel Tuka (Bosnia and Herzegovina), Ryan Sanchez (Puerto Rico) na Marcin Lewandowski (Poland) walifagia nafasi tatu za kwanza.

Nelly Jepkosgei pia hakuwa na lake katika mbio za mita 800 alipolazimika kuridhika na nafasi ya tatu nyuma ya Muamerika Ajee Wilson na Muethiopia Habitam Alemu katika kitengo kilichovutia wakiambiaji 10.