Michezo

Riadha za Dunia: Cherotich, Yavi na Chemutai wembe makundi ya 3,000m kuruka viunzi na maji

Na GEOFFREY ANENE September 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

BINGWA wa dunia na Olimpiki, Winfred Yavi kutoka Bahrain, mshindi wa shaba ya Olimpiki na dunia, Faith Cherotich wa Kenya, pamoja na bingwa wa Olimpiki na mshindi wa fedha ya dunia, Peruth Chemutai wa Uganda, walifuzu fainali ya mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwenye Riadha za Dunia mjini Tokyo, Japan, Jumatatu.

Watatu hao walitawala makundi yao ya mchujo katika nusu-fainali. Katika mchujo wa kwanza, Cherotich alionyesha ubabe alipotumia dakika 9:13.95 kumaliza nambari moja na kufuzu moja kwa moja.

Cherotich akishinda mchujo wake. PICHA | REUTERS

Wengine katika kundi hilo waliofuzu naye ni bingwa wa dunia wa 2022, Norah Jeruto kutoka Kazakhstan (9:14.25), Muingereza Elise Thorner (9:14.37), Mfaransa Flavie Renouard (9:14.69) na Mwamerika Lexy Halladay (9:15.06).

Mkenya mwingine, Celestine Biwot, hakufua dafu baada ya kumaliza katika nafasi ya saba kwa dakika 9:22.55 na hivyo kuaga mashindano.

Mchujo wa pili ulishuhudia Yavi – aliyezaliwa Kenya kabla ya kubadili uraia kuwa wa Bahrain – akiongoza kwa 9:15.63. Alimzidi maarifa Mtunisia Marwa Bouzayani (9:15.68), Muethiopia Sembo Almayew (9:15.84), Mjerumani Gesa Krause (9:16.76) na Mwamerika Angelina Napoleon (9:18.03) waliofuzu pia.

Hata hivyo, Pamela Kosgei wa Kenya alimaliza nambari 10 kwa dakika 9:28.21 na hivyo kubanduliwa.

Doris Lemngole pia afuzu fainali

Katika mchujo wa tatu, Chemutai alinyakua ushindi kwa 9:07.68, huku Mkenya Doris Lemngole akijikatia tiketi kwa kuwa nambari mbili katika muda wa dakika 9:08.97.

Wakimbiaji wengine waliomaliza kundi hilo tano-bora na kutinga finali ni Muethiopia Lomi Muleta (9:12.20), Mjerumani Lea Meyer (9:13.18) na Mwamerika Kaylee Mitchell (9:15.52).

Doris Lemngole akishiriki mchujo wake Jumatatu. PICHA | REUTERS

Kwa sasa, Yavi, Cherotich, Chemutai, Almayew na Jeruto wanaorodheshwa miongoni mwa sita-bora duniani katika mbio hizo za 3,000m kuruka viunzi na maji katika usanjari huo.

Rekodi ya dunia bado inashikiliwa na Mkenya Beatrice Chepkoech ya dakika  8:44.32 aliyoweka Julai 20, 2018. Jeruto naye anamiliki rekodi ya Riadha za Dunia ya dakika 8:53.02 tangu mwaka 2022.

Mashabiki wanasubiri kwa hamu fainali hapo Septemba 17, ambapo rekodi hizo zinaweza kufutwa; Yavi akiwa na muda bora zaidi msimu huu (8:45.25), akifuatwa na Cherotich (8:48.71) na Chemutai (8:51.77).