Michezo

Riara University FC kujituma kuingia KPL

December 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA JOHN KIMWERE 

INGAWA ni timu changa inapania kupambana mwanzo mwisho kuhakikisha inashusha soka ya kutesa ili kutwaa tikiti ya kushiriki kugaragaza gozi ya Ligi Kuu ya KPL miaka ijayo.

Aidha, Riara University FC ni kati ya vikosi vya Vyuo Vikuu ambavyo kando na michezo baina ya vyuo pia vinashiriki mechi za Ligi ambazo huandaliwa na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF).

Kocha wake mkuu, Owen Makokha anasema tayari safari ya kushiriki soka ya haiba ya juu nchini imeng’oa nanga baada ya kunasa tikiti ya kushiriki kipute cha Nairobi West Regional League (NWRL) muhula huu.

”Mafanikio yetu kwenye mechi za kipute cha Ligi ya Kaunti ya Nairobi msimu uliyopita ni dhihirisho kwamba tumeanza mwendo wa kusonga mbele kwenye kampeni za soka ya hapa Kenya,” anasema na kuongeza kuwa wanafahamu fika katika ngarambe hiyo kamwe hakuna mteremko.

Kadhalika anadokeza kuwa ana mpango kabambe kwa vijana wake ndani ya miaka mitano ijayo kuhakikisha wanaendelea kufanya kweli.

Aliongeza “Nina imani tosha tutafanya vizuri kwenye migarazano ya kuwania ubingwa wa taji hilo msimu huu.”

Riara University ilinasa tikiti ya kufuzu kupandishwa ngazi baada ya kumaliza kati ya tano bora kwa kuzoa pointi 34 kwenye msimamo wa mechi za Kundi A Ligi ya Kaunti ya msimu uliyopita.

Baadhi ya wanasoka wa KYSA Karengata FC inayoshiriki kipute hicho.

Riara University FC inajivunia kujumuisha wachezaji wepesi ambao tayari wameonyesha wanapania makubwa katika soka ya humu nchini akiwamo Jamal Jamaa (nahodha), Michael Jefwa, Fidel Sena, Collins Khisa, Patrick Lopanu,Cliff Kisero, Leroy Alushula, Brian Tarus, Jeremiah Ochiel na Vitalis Khaemba.

Wengine ambao wamo katika orodha ya wachana nyavu wanaounda kikosi hicho wakiwa Kyalo Ngola, Joram Magero, Kennedy Mwenda, Carlos Karuga, Zakaria Ngavala, Simon Masinde, Hillary Nyapande na Arnold Alushula. Pia wapo Walukho Wasilwa, Mohamed Ali, Peter Mungai, Ronald Odhiambo, Sammy Chone, Abdulfatah Bonaya na Allan Kipkemoi.

Naye nahodha wake anasisitiza kuwa Chuo cha Riara kimezamia juhudi za kusaka wafadhili ili kukipiga jeki kuelekea mpango wa kuanzisha kuanzisha mpango wa kutoa ufadhili kwa wanafunzi waliotunukiwa kipaji cha kusakata boli kuendeleza elimu katika chuo hicho.

Juhudi za mradi huo zinadhihirisha kuwa chuo hicho kimepania kuibuka kati ya vituo vya kukuza wanasoka chipukizi nchini.

Riara University FC ambayo hutumia uwanja wa Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) pia ina imani tosha kwamba imejiweka pazuri katika soka ya kinyang’anyiro hicho pia itakuwa ikifanya vizuri kwenye mashindano ya vyuo vikuu nchini.

Anashukuru uongozi wa chuo hicho kwa kuwaunga mkono hasa kugharamia mahitaji yao kwenye kampeni za michezo ya ligi ya FKF wanaoshiriki kwa mara ya kwanza mwaka huu. Anawaambia wanasoka wake kuwa hawana budi wanastahili kujituma zaidi bila kulaza damu

kampeni za kipute hicho ili kufuzu kusonga mbele muhula ujao.

Kadhalika anaamini jinsi wameanza kupanda daraja ndivyo wachezaji wake wanavyozidi kutambuliwa na kuteuliwa kuchezea timu zinazoshiriki ligi za juu nchini.