Michezo

Ronaldo atinga hatua muhimu maishani kwa kufikisha mabao 900

Na JOHN ASHIHUNDU NA MASHIRIKA September 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

CRISTIANO Ronaldo alifika hatua muhimu Alhamisi usiku, Septemba 5, 2024 baada ya kufunga bao la 900, huku akisaidia Ureno kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Croatia katika mechi ya UEFA Nations League, ugani Estadio da Luz, Ijumaa usiku.

Mara tu baada ya kufunga bao hili dakika ya 34, nyota huyo mwenye umri wa miaka 39 alikimbia kwenye kona moja uwanjani humo na kupiga magoti huku akiangua kilio kihisia.

Bao hilo lilikuwa la 131 kufungia nchi yake, baada ya hapo awali kufungia klabu za Sporting Lisbon, Manchester United, Real Madrid, Juventus na sasa Al-Nassr ya ligi kuu nchini Saudi Arabia.

“Nilisherehekea kwa hisia kwa sababu lilikuwa bao la muhimu maishani mwangu,” alisema mshambuliaji huyo. “Nashukuru kikosi kizima kwa bao hili la kihistoria. Ni bao la kipekee katika maisha yangu ya kusakata soka,” alisema staa huyo ambaye amecheza mpira kwa zaidi ya miaka 20.

Ronaldo aliifungia Sporting Lisbon mabao mawili akiwa na umri wa miaka 17 mnamo 2002 katika ushindi wao wa 3-0 dhidi ya Moreirense.

Aliyoyomea kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na kufungia Manchester United mabao 118 katika mechi 293 kabla ya kujiunga na Real Madrid mnamo 2009 kwa mkataba uliogharimu Sh13.5 Bilioni.

Akiwa huko kwa kipindi cha miaka tisa, Ronaldo aliwafungia vigogo hao wa La Liga mabao 450 katika mechi 438 kabla ya kujiunga na Juventus na kuwafungia vigogo hao wa Serie A mabao 101 katika kipindi cha miaka mitatu, kabla ya kuamua kurejea United na kufunga 27 katika mechi 54.

Hata hivyo, kurejea kwake Red Devis hakukumpa sifa alizopata katika kipindi cha awali, ikabidi aamue kwenda Saudi Arabia mnamo 2023 kujitafutia mihela, ambapo kufikia sasa amefunga mabao 68.

Nusu ya mabao yake (437) aliyafunga mara tu alipofikisha umri wa miaka 30 mnamo Februari 2015.

Kwenye mabao yake 900, 164 yalipatikana kupitia kwa mikwaju ya penalti, 64 yakipatikana kupitia kwa fri-kiki.

Mabao 768 aliyafunga akiwa ndani ya kijisanduku, 132 akiwa nje ya kijisanduku, huku akijivunia hat-tricks 66.

Alifunga mabao 479 akichezea nyumbani; 361 akiwa ugenini; 60 akiwa katika viwanja visivyo na upande.

Mabao mengi aliyofunga ni dhidi ya Sevilla (27), Atletico de Madrid (25), Getafe (23), Barcelona (20) na Cela de Vigo (20).

Hakuna utafiti halisi uliofanywa, lakini Ronaldo anaonekana kuongoza orodha ya ufungaji mabao Duniani, baada ya kuzima rekodi ya awali ya mabao 800.

Kuna madai kwamba majagina Pele na Romario walifunga zaidi ya mabao 1,000 kila moja, lakini mabao ya mechi za kirafiki ikitolewa wanabaki na 700 kila mmoja.

Utafiti usiothibitika unaonyesha Pele akiwa na mabao 778, huku Romario akiwa na 785.

Mpinzani wake mkuu, Lionel Messi amefunga 867 kufikia sasa.

Huenda nahodha huyo wa Ureno analenga kufunga mabao 1000 ndipo astaafu, baada ya majuzi kusema hatarajii kustaafu hivi karibuni.

Wengi wanamtarajia kustaafu akiwa na umri wa miaka 40 baada ya kucheza katika fainali za Kombe la Dunia la 2026.