Michezo

Ronaldo awika huku Ureno ikiteswa mechi ya kusaka tiketi Euro

October 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

KYIV, UKRAINE

MSHAMBULIAJI Cristiano Ronaldo alifunga bao lake la 700 katika taaluma yake ya kucheza soka alipopachika wavuni mkwaju wa penalti dakika ya 72 katika pambano la Euro 2020 ambalo timu yake ya Ureno ilishindwa 2-1 na Ukraine, ugenini.

Mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 34 ameifungia timu ya taifa mabao 95, mbali na mengine 450 akiwa na Real Madrid, 118 (Manchester United), 32 (Juventus) na matano (Sporting Lisbon).

Kichapo hicho cha 2-1, kinamaanisha Ukraine imefuzu kwa fainali hizo za bara Ulaya baada ya kuongoza Kundi B kwa pointi 19 kutokana na mechi saba, kwa mwanya wa pointi nane mbele ya Ureno, ambao wamecheza mechi chache.

Ureno ambao wamejikusanyia jumla ya pointi 11 kutokana na mechi sita watacheza na Lithuania na baadaye kumalizana na Luxembourg.

Serbia wanaoshikilia nafasi ya tatu kwa pointi 10 kutokana na mechi sita waliandikisha ushindi wa 2-1 dhidi ya Lithuania.

Luxembourg wana pointi nne kutokana na mechi sita, huku Luxembourg wakishikilia nafasi ya mwisho kwa pointi moja baada ya kucheza mechi saba.

Jijini Kyiv, mabao ya mapema kutoka kwa Roman Yaremchuk na Andriy Yarmolenko yaliiwezesha Ukraine kuongoza kwa 2-0 dhidi ya Ureno kabla ya Ronaldo kufunga penalti na kufanya mambo kuwa 2-1. Taras Stepanenko wa Ukraine alipigwa kadi nyekundu kwa kucheza ngware.

Wakati huo huo, Ufaransa itasubiri kufahamu hatima yake kwenye michuano hiyo baada ya kulazimishiwa sare ya 1-1 dhidi ya Uturuki. Kaan Ayhan alisawzisha zikibakia dakika nane, wakati Ufaransa walikuwa juu kwa bao la Olivier Giroud.

Uturuki wanaongoza Kundi hilo la H wakiwa na pointi 19 kutokana na mechi nane, mbele ya Ufaransa kutokana na ushindi wao wa mabao 2-0 hapo awali jijini Konya mwezi Juni.

Iceland ambao waliandikisha ushindi wa 2-0 dhidi ya Andorra wanakamata nafasi ya tatu katika kundi hilo baada ya kujikusanyia jumla ya pointi 15. Albania ambao waliibuka na ushindi wa 4-0 dhidi ya Moldova, wanashikilia nafasi ya nne wakiwa na pointi 12.

Katika mechi nyingine ya Kundi A, Kosovo waliandikisha ushindi wa 2-0 dhidi ya Montenegro katika mjini Pristina.

Mabao ya kupachikwa mapema

Mabao ya mapema kupitia kwa Amir Rrahmani na Vedat Mariqi yamewawezesha washindi kukaribia Jamhuri ya Czech ambao wanakamata nafasi ya pili kundini humo. Timu hizo zitakutana jijini Prague hapo Novemba 14.

Uingereza ambao ndio vinara wa kundi hilo, watafuzu mapema iwapo wataibwaga Montenegro katika mechi itakayochezewa Wembley, pia siku hiyo.

Kocha wa Uingereza, Gareth Southgate anaamini baada ya mkubwa, wa mabao 6-0 dhidi ya Bulgaria mnamo Jumatatu usiku, siku chache tu baada ya kupokea kichapo cha 2-1 kutoka kwa Jamhuri ya Czech, mwishoni mwa wiki vijana wake hawakamatiki.

Hata hivyo, mkufunzi huyo alielezea kuudhika na vitendo vya kibaguzi kutoka kwa mashabiki wa Bulgaria walioendelea kuwafokea wachezaji wa asili ya Kiafrika Tyrone Mings, Raheen Sterling na Marcus Rashford.

Wakati mmoja, mwamuzi Ivan Bebek aliusimamisha mchezo dakika ya 41 kutokana na vitendo hivyo ambapo kocha Southgate alikaribia kuwaondoa vijana wake uwanjani.