Rooney wa Man U apeleka ‘nuksi’ ya vichapo Birmingham na kwa hilo amefutwa
NA LABAAN SHABAAN
MENEJA wa Birmingham City Wayne Rooney amemwaga unga baada ya kuwa kocha kwa siku 83 tu katika klabu hiyo ya daraja la pili nchini Uingereza.
“Kwa bahati mbaya, muda wa Wayne kuwa nasi haukuenda kama tulivyopanga na tumeamua kufuata mkondo mwingine,” ilisema sehemu ya taarifa ya Birmingham City ya Januari 2, 2024.
Kisha klabu hiyo ikasema: “Mchakato wa kumtafuta mrithi mwingine umeanza mara moja na tutawaarifu mashabiki wetu tutakapokuwa na habari zaidi.”
Tangu alipomwaga wino kwenye mkataba mpya mnamo Oktoba 11, 2023 ili kuwanoa wachezaji hao, Rooney alisimamia mechi 15 na kupigwa mara 9 akiibuka sare mara 4 huku akishinda mara 2.
Mchezaji huyo lejendari wa miamba wa Uingereza na Manchester United, alianza kazi wakati klabu hiyo ilikuwa nafasi ya 6.
Ameishia kupigwa kalamu kikosi hicho kikiwa nambari 20 kwenye jedwali la ligi hiyo.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 38 alipokea mikoba ya uongozi kutoka kwa John Eustace aliyeonyeshwa mlango katika hali tatanishi.
“Kandanda ni biashara ya matokeo na ninatambua wachezaji hawa hawajakuwa katika viwango nilivyotaka wawe,” Rooney alisema.
Kocha wa ustawishaji wachezaji kitaaluma Steve Spooner atakuwa kaimu Mkufunzi wa Birmingham.
Ni dhahiri kuwa kutimuliwa kwake Rooney kumemwathiri sana sababu amesema itamchukua muda kusahau athari ya uamuzi huu dhidi yake.
“Lakini, muda ni kitu cha thamani sana ambacho meneja anahitaji na siamini wiki 13 zilitosha kusimamia mabadiliko yaliyohitajika,” alijuta baina ya kutoa shukurani kwa uongozi wa Birmingham City.
Mchezaji huyo wa zamani wa The Red Devils ndiye kocha aliyehudumu kwa muda mfupi sana katika klabu ya Blues.