Michezo

Rosemary Wanjiru alenga Olimpiki

July 21st, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

MWANARIADHA Rosemary Wanjiru sasa analenga kujizolea medali ya Olimpiki baada ya kupata hamasa kutokana na ushindi wa mbio za mita 10,000 kwenye duru ya tatu ya kivumbi cha Hokuren Distance Challenge mjini Abashiri, Japan.

Wanjiru alizitamalaki mbio hizo siku 10 baada ya kufungua kampeni za msimu wa huu wa 2020 kwa ushindi mwingine mkubwa katika mbio za mita 5,000 mjini Fukagawa, Japan.

Wanjiru alikamilisha mbio za Hokuren katika muda wa dakika 30:38.18, sekunde 45 zaidi mbele ya Mao Ichiyama wa Japan aliyeambulia nafasi ya pili kwa muda wa dakika 31:23.30. Huo ulikuwa muda wake bora zaidi kwa Ichiyama kusajili msimu huu.

Wanjiru alikosa sekunde tatu pekee kuandikisha muda wake bora zaidi msimu huu kuliko ule wa dakika 30:35.08 aliouweka katika mbio za mita 10,000 kwenye Riadha za Dunia mwaka jana jijini Doha, Qatar. Alidhibiti uongozi wa mbio hizo mapema na akasalia kufuatwa na wanariadha wawili pekee: Ichiyama na Mizuki Matsuda wa Japan kufikia hatua ya mita 1,000 za mwanzo baada ya dakika 3:08 pekee.

Ichiyama anatarajiwa kutoana jasho na Wanjiru kwa mara nyingine atakapokuwa akinogesha Olimpiki zijazo jijini Tokyo, Japan. Michezo hiyo ya Olimpiki iliahirishwa hadi mwakani kwa sababu ya ugonjwa wa Covid-19 japo waandalizi wamedokeza mpango wa kuiahirisha zaidi.

Wanjiru aliyetinga hatua ya mita 5,000 baada ya dakika 15:24 pekee. Aliwahi kuandikisha muda wa dakika 29:50 mnamo 2018, huu ukiwa muda wa tatu wa kasi zaidi kuwahi kusajiliwa katika historia ya mbio za mita 10,000.

Kwa upande wa wanaume, Jonathan Ndiku anayejulikana sana kwa ubabe wake katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji, alitamalaki mbio za mita 10,000 na kuibuka mshindi baada ya dakika 27:23.47. Aliwahi kutwaa ubingwa mara mbili katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji miongoni mwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20. Alifuatwa kwa karibu na Wakenya Alexander Mutiso (27:44.37) na Richard Kimunyan Yator (27:49.35).

Yuma Hattori ambaye pia atapeperusha bendera ya Japan kwenye Olimpiki zijazo za Tokyo, aliambulia nafasi ya nne kwa muda wa dakika 27:56.32. Alikosa sekunde 13 pekee kufikia muda wake bora aliouandikisha miaka mitano iliyopita.

Bingwa wa dunia katika mbio za mita 3,000 kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20, Nozomi Tanaka alimzidi maarifa Mkenya Hellen Ekarare (15:03.09) katika mbio za mita 5,000 na kuibuka wa kwanza baada ya muda wa dakika 15:02.62.

Bernard Kibet Koech aliibuka mshindi wa mbio za mita 5,000 kwa upande wa wanaume baada ya muda wa dakika 13:11.77.