Rupp na Mo Farah kumenyana na Wakenya Chicago Marathon
Na GEOFFREY ANENE
LICHA ya majina makubwa Geoffrey Kirui, Dickson Chumba na Abel Kirui kutoka Kenya kuwa katika orodha ya washiriki watakaotimka katika mbio za Chicago Marathon hapo Oktoba 7, 2018, vita vya taji vimetabiriwa vitakuwa vikali kati ya Mwamerika Galen Rupp na Muingereza Mo Farah.
Wakenya Bernard Kipyego na Kenneth Kipkemoi pia watashiriki makala haya ya 41, ambayo yamevutia washiriki 45, 000 kutoka zaidi ya mataifa 100. Rupp atatetea taji ambalo alishinda mwaka 2017 kwa saa 2:09:20, sekunde 28 mbele ya Abel Kirui naye Kipyego alifunga tatu-bora kwa saa 2:10:23.
Geoffrey Kirui ni bingwa wa dunia na Boston Marathon mwaka 2017 naye Chumba ni mfalme wa Tokyo Marathon mwaka 2014 na 2018. Chumba alinyakua taji la Chicago Marathon mwaka 2015. Abel Kirui alifuata nyayo za Chumba kwa kuibuka mshindi mjini Chicago mwaka 2016, mara ya mwisho Mkenya alishinda katika mji huu.
Kenneth Kipkemoi alitwaa taji la Rotterdam Marathon nchini Uholanzi mwezi Aprili mwaka 2018. “Kutakuwa na ushindani mkali sana katika kitengo cha wanaume, ingawa vita vitakuwa vikali zaidi kati ya Galen Rupp na Mo Farah.
Kukutanishwa kwa wanafunzi hawa wa zamani wa kocha Alberto Salazar kunasisimua zaidi kuliko washiriki wengine. Rupp bado ananolewa na Salazar na katika timu ya Nike Oregon Project, lakini Farah anafunzwa na Gary Lough, mume wa Paula Radcliffe, tangu aachane na mbio za uwanjani na kujitosa katika mbio za barabarani mwaka mmoja uliopita,” tovuti ya FloTrack inasema.
Shujaa wa mbio za uwanjani Farah aliridhisha katika London Marathon mnamo Aprili mwaka 2018 alipotimka kwa saa 2:06:21 na kumaliza katika nafasi ya tatu nyuma ya Mkenya Eliud Kipchoge (2:04:17) na Shura Kitata (2:04:49).
Mbali na Rupp na Farah, Wakenya watapimwa vilivyo kasi yao dhidi ya bingwa wa Boston Marathon Yuki Kawauchi kutoka Japan na Waethiopia Mosinet Geremew na Birhanu Legese.