Michezo

Rush United inavyokuza soka Nakuru

March 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MAOSI

Dhana potovu kuwa soka za mitaani hazina mashiko imepitwa na wakati. Hii ni kwa sababu wachezaji nyota wamekuwa wakiibuka kutoka mashinani mara nyingi katika mitaa ya mabanda.

Kwa mfano Victor Wanyama anayecheza soka ya kulipwa ulaya ni mzawa wa Muthurwa Nairobi, lakini azma ya kusakata soka ulaya kwa timu ya Tottenham haikuzima.

Mjini Nakuru timu kama vile Nakuru All Stars, St Joseph, Bondeni Youth , Nakuru West Queens ( ambao sasa wanashiriki ligi ya akina dada nchini (KWPL) ni baadhi ya talanta za kupigiwa mfano miongoni mwa vijana.

Mfano mzuri ni kikosi cha Rush United FC kinachojivunia wanasoka shupavu wenye tajriba pana katika ulingo wa soka katika viwango mbalimbali.

Baadhi yao ni kama vile Dan Sunguti na Elvis Rupia wanaojaza kikosi cha kwanza soka ya kulipwa katika ligi ya KPL na timu ya AFC Leopards.

Dimba iliwatembelea katika uwanja wa Afraha Nakuru, kutadhmini kwa kina mbinu za kiufundi zinazotumika kutambisha kikosi cha Rush United FC.

Wachezaji wa Rush United walijumuika na wachezaji hawa wa kitambo kushuhudia mechi ya Betway dhidi ya Ushuru FC ambapo AFC walishinda.

Nahodha Ian Kibet anayechezea U-13 anasema soka imempatia uwezo wa kutangamana na wachezaji kutoka timu zingine ndani na nje ya Nakuru.

Alieleza kuwa kabumbu imekuwa ikitoa fursa safi kwake kupitiza muda kwa njia ya hekima na busara kuliko kushinda mchana kutwa akitazama filamu tu.

“Ninawahimiza wanafunzi wengine wenye talanta ya kucheza mpira watumie muda wao kufanya mazoezi na kucheza mpira ili kuboresha afya yao,”asema.

Mkufunzi Edward Kwintira anasema mafanikio ya timu yake ni kutokana na juhudi za wachezaji kushirikiana ili kuandikisha matokeo mazuri.

Aidha wazazi wamekuwa mstari wa mbele kupiga jeki soka ya kabumbu miongoni mwa Watoto wao, kwa kuwaruhusu washiriki mazoezi kila siku za wiki baada ya masomo, mechi za kirafiki na zile za shirikisho la FKF tawi la Magharibi ukanda wa kati.

Edward anasema kupiga magoli mengi kila msimu na wachezaji kufanya mazoezi ya kutosha ndio nguzo muhimu kwa mafanikio ya timu yake.

Alieleza kuwa anawategemea washambulizi mara nyingi anapolenga kutwaa taji au pale anapotafuta ushindi muhimu wa kujiongezea alama katika jedwali.

Ingawa washikadau hawajawekeza kikamilifu katika mchezo wa soka, wachezaji wake wamejinyima angalau kupata Mabuti, jezi, nyavu na uwanja wa kushiriki mechi za nyumbani.

Aidha wanatumia mfumo wa timu zilizokubuhu katika soka ya 4-3-2-1, mfumo ambao ni wa kukaba na kushambulia sawia huku wepesi wa wachezaji ukileta tija kubwa katika kambi ya wanasoka hawa chipukizi.

Timu ya Rush inamiliki timu ya akina dada na wavulana wa U-10,U-13,-15,U-18 na U-20 zote zikitumika kama daraja ya kuvuka kutoka kiwango kimoja cha soka hadi kiwango kingine.

“Rush United imekuwa ikiandaa michuano ya Back to School, ili kuwaleta wachezaji wenye uwezo tofauti kutoka mitaani waonyeshe vipaji vyao katika ulingo wa soka,” akasema.

Hali hii imesaidia jamii kwa jumla kupigana na swala la mihadarati na kuwahimiza Watoto kuhudhuria masomo yao, hii ikiwa ni njia mojawapo ya kujiendeleza kimaisha siku za baadae.

Edward anasema soka ya humu nchini inaendelea kuku ana anashauri wizara ya michezo kuwekeza vilevile katika soka za mitaani ambazo zimesahaulika.

Mbali na nyumbani wamekuwa wakicheza katika uwanja wa Kamukunji dhidi ya Galactico FC na Bondeni Youth na kuandikisha jumla ya matokeo mesto huku wakiibuka kidedea kwa mechi mbili na kupiga sare moja.

Edward anasema analenga kuwapatia wachezaji wake tajriba ya kutosha ili waje kuwa nguzo muhimu kwa timu ya Taifa Harambe Stars na Harambee Starllets.

Anaona kuwa wengi wao watakuja kusakata soka katika kiwango cha kimataifa kama vile kwa timu zilizokubuhu za Liverpool, Chelsea, Manchester United na Tottenham.