Ruto aibia AFC Leopards ujanja wa kujizolea mkwanja
NA JOHN ASHIHUNDU
RAIS William Ruto ameshauri wanachama wa AFC Leopards wabadilishe klabu hiyo ili iwe shirika lenye faida badala ya kuendelea kuwa timu ya kijamii.
Wakati huo huo, kiongozi huyo wa taifa ametoa changamoto kwa viongozi wa klabu hiyo kuhakikisha maslahi ya wachezaji yanapewa kipaumbele.
Alisema iwapo watakubalia kufanya mabadiliko hayo, klabu hiyo itavutia wawekezaji wengi kutokana na ufuasi mkubwa wa timu hiyo nchini na katika mataifa ya kigeni.
“Ili mpige hatua, itabidi mkubali kubadilisha hii timu ili iwe shirika lenye faida badala ya kuendelea kuwa mali ya jamii,” Ruto alitoa ushauri huo Jumatano usiku baada ya kukutana na maafisa wa klabu hiyo, kamati andalizi ya sherehe za Ingwe@60, pamoja na mashabiki kadhaa waliomtembelea Ikulu.
Rais Ruto aliyeahidi kuhudhuria kilele cha sherehe hizo uwanjani Nyayo mnamo Machi 24, 2024, kadhalika aliitaka klabu hiyo ifuatilie ardhi waliyopewa na marehemu Rais (mstaafu) Daniel arap Moi mnamo 1992 karibu na uwanja wa kimataifa wa Moi, Kasarani.
Rais Ruto alisisitiza umuhimu wa michezo kuwapa vijana kazi, huku akiongeza kwamba michezo katika ubia si muda wa kupitia tena.
“Ni jukumu letu kama viongozi kuhakikisha vijana wanapata haki yao kutokana na jasho wanalotoa wakishiriki michezo,” akashauri.
Mkutano huo vile vile ulihudhuriwa na Waziri wa Michezo Ababu Namwamba, mwenyekiti wa Leopards Dan Shikanda na viongozi wengi wa klabu hiyo, mlezi wa klabu hiyo Alex Muteshi pamoja na mwenyekiti wa kamatiandalizi ya Ingwe@60, Vincent Shimoli.
AFC Leopards maarufu kama Ingwe inaadhimisha mika 60 tangu ianzishwe 1964 katika Ukumbi wa Kaloleni, Nairobi, lakini imekuwa ikipitia katika wakati mgumu sawa na klabu nyingine za kijamii kama Gor Mahia na Shabana FC.
Leopards ambayo ni miongoni mwa timu zilizo na sifa tele inajivunia mataji 12 Ligi Kuu, vikombe 10 vya Kenya Cup, na ushindi mara tano wa Klabu Bingwa kanda ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).
Miaka ya 1970s na 1980s inaonekana kuwa ya ufanisi zaidi kwa klabu hiyo ambayo ilitwaa mataji ya ligi kuu mnamo 1966, 1967, 1970, 1973, 1980, 1982, 1986, 1988, 1992 na 1998, lakini tangu wakati huo imekaa miaka 22 bila kushinda taji hilo.
Leopards iliwahi kuteremshwa mnamo 2006 lakini ikarejea 2009, mwaka ambao pia walitwaa ubingwa wa Kenya Cup sasa FKF Cup.