Michezo

Saa ya Sh233 milioni ya Rudiger yaleta noma, akiri mama watoto hasemi naye

June 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA CHRIS ADUNGO

BEKI mzoefu wa Real Madrid, Antonio Rudiger, alisherehekea ushindi wao wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kwa kuvalia saa ya thamani ya Sh233.8 milioni!

Real walijizolea taji la 15 la UEFA Jumamosi iliyopita baada ya kupepeta Borussia Dortmund 2-0 ugani Wembley, Uingereza.

Rudiger, 31, ambaye awali alinyanyua kombe hilo akiwa Chelsea mnamo 2021, alikuwa sehemu ya kikosi kilicholeta Real ufanisi huo.

Kilichovutia mashabiki zaidi Los Blancos wakinyanyua UEFA wikendi jana ni saa ya Rudiger ambayo sasa inatisha kuyumbisha ndoa yake na Laura.

Akihojiwa na gazeti la The Sun wiki hii, sogora huyo alikiri kuwa vidosho wengi wamekuwa wakimvizia mitandaoni wakitaka fursa ya kutoka naye kimapenzi tangu watie machoni saa hiyo ghali.

“Ni kama wanahisi nina mihela. Pengine saa yenyewe iliwavutia mno. Wajue Laura hajafurahishwa kabisa nao. Jumbe na simu zao zinavuruga amani, japo naamini mambo yatatulia,” alisema Rudiger.

Laura, 29, ni mama wa watoto wawili na mchezaji wa zamani wa handiboli katika timu ya taifa ya Ujerumani. Alianza kumburudisha Rudiger kimapenzi mnamo 2015 na uhusiano wao umejaliwa watoto wawili – Djamal Sahr na Aaliyah Trophy aliyezaliwa 2021.

Kulingana na mtandao wa Insaneluxurylife, saa ya Rudiger ni ya aina ya Nautilus 5711/1A-018. Jumla ya 170 pekee zimewahi kutengenezwa na kuuzwa kwa bei ya awali ya Sh7.5 milioni.

Walakini, kwa sababu ya uchache wake bei ilipanda sokoni hadi kufikia Sh233.8 milioni kwa sasa.

Hiyo ni takwimu ya kushangaza ikizingatia kuwa kombe la UEFA ambalo Rudiger alinyanyua wikendi iliyopita ni la thamani ya Sh7.2 milioni pekee.

Mchezaji wa zamani wa NBA, LeBron James, ni miongoni mwa watu wachache wanaomilika saa ya Nautilus 5711/1A-018. Alionekana akiwa ameivalia kwenye mashindano ya magari ya 24 Hours of Le Mans nchini Ufaransa mwaka jana.

Rudiger, ambaye ameichezea Ujerumani mara 68, alijiunga na Real bila mnamo 2022 baada ya mkataba wake Chelsea kutamatika.

Tayari ametandaza zaidi ya mechi 100 kambini mwa miamba hao wa Uhispania na kunyanyua mataji mengi ya haiba katika kipindi cha miaka miwili.

Anajiandaa sasa kuongoza wenyeji Ujerumani kwenye fainali za Euro 2024.