Michezo

Sababu ya Equity kuangusha benki zingine michezoni

October 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

TIMU za wafanyakazi wa benki ya Equity kando na masuala ya fedha wameonyesha bayana kwamba pia michezoni sio wachache.

Timu za Equity Bank (wanaume na wanawake) zilipambana na ushindani mkali dhidi ya washiriki wengine na kuibuka mabingwa wa michezo baina ya Mashirika ya Kifedha nchini makala ya mwaka huu iliyofanyika katika uwanja wa KSMS, Nairobi.

Afisa wa Equity Bank, Joseph Wachira Waruru akituzwa kombe na Waziri wa Michezo, Amina Mohamed baada ya kuibuka mabingwa katika Michezo ya Mashirika ya Kifedha. Picha/ John Kimwere

Wanamichezo hao walitawazwa mabingwa baada ya kukusanya jumla pointi 1075 kutoka zaidi ya fani kumi walizoshiriki.

Nao wenzao wa Central Bank of Kenya (CBK) waliokuwa mabingwa watetezi waliteleza na kuibuka mbili bora kwa alama 1071. Nayo Barclays Bank of Kenya (BBK) iliyomaliza ya pili mwaka uliopita ilizoa alama 1010 na kumaliza tatu bora.

Nao wanamichezo wa Co-operative Bank na KCB walipata pointi 981 na 968 na kumaliza nafasi ya nne na tano mtawalia.

Afisa wa CBK, Ezekiel Tanui akipokezwa kombe na Waziri wa michezo, Amina Mohamed baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye Michezo ya Mashirika ya Kifedha. Picha/ John Kimwere

Equity Bank ilionyesha ushujaa wake huku ikijivunia kubeba taji hilo mwaka 2016, pia kumaliza nafasi ya pili na tatu mwaka 2017 na 2018 mtawalia.

Equity ilitawazwa wafalme wa ngarambe hiyo baada ya kukazana kwa udi na uvumba na kuibuka kati ya nafasi tatu za kwanza katika fani tofauti.

Katika soka la wanaume Equity ilihifadhi taji hilo ilipoigonga KCB mabao 4-1 katika fainali. Kitengo cha wanawake, Equity iliibuka malkia iliposajili alama kumi baada ya kushinda mechi tatu kwa goli 1-0 kila moja, kutoka nguvu sare tasa dhidi ya BBK.

Afisa wa BBK akituzwa kombe na Waziri wa michezo, Amina Mohamed baada ya kumaliza nafasi ya tatu kwenye Michezo ya Mashirika ya Kifedha. Picha/ John Kimwere

Kisha ilijikuta njiapanda ilipokubali kulala goli 1-0 na CBK. ”Sina shaka kupongeza timu zote mbili kwa kuonyesha mchezo safi na kubeba taji la mwaka huu ambapo haikuwa rahisi hasa kitengo cha wanaume kuhifadhi ubingwa huo,” alisema meneja wa Equity, Ben Juma.

Kwenye mpira wa mikono, Equity iliionyesha ubabe wake na kutwaa ubingwa huo mbele ya CBK na Co-operative Bank zilizoibuka nafasi ya pili na tatu mtawalia.

Nahodha, Bernadette Ngochi wa timu ya wanawake ya CBK ya kuvuta kamba (Tug of War) akituzwa kombe na Ezekiel Tanui kwa kuibuka mabingwa katika mashindano ya mwaka huu. Picha/ John Kimwere

Aidha ilimaliza ya pili kwenye mchezo wa kurusha vishale na Snooker. Katika fani hizo mbili, wachezaji wa timu za CBK) walitawazwa mabingwa baada ya kushusha upinzani wa kufa mtu na kuwazidi wenzao ujanja.

Katika riadha ya wanaume Equity Bank ilishindwa kufana na kukosekana katika nafasi tatu za kwanza ambapo ubingwa uliendea CBK huku Postbank na KCB zikimaliza mbili na tatu bora mtawalia.

Katika riadha ya wanawake Postbank iliendelea kutawala sawa na makala zilizopita huku Equity ikiibuka ya pili mbele ya KCB.

Nahodha, Moses Ong’aro wa timu ya wanaume ya CBK katika mchezo wa Squash akituzwa kombe na Ezekiel Tanui kwa kuibuka mabingwa katika mashindano ya mwaka huu. Picha/ John Kimwere

Hata hivyo kitengo cha wanaume mbio za mita 1500, Lewis Kamau wa Equity alimaliza wa kwanza, nao Silas Tanui na Vincent Langat wa BBK na CBK walikamata nafasi ya pii na tatu mtawalia.

Mbio za Mita 100, Aley Mwangi wa Equity alibeba ubingwa alipotimka kwa dakika 11.5, nafasi ya pili na tatu ziliendea Noah Kigen na Morgan Rangita wote KCB kwa muda wa dakika 11.9 na 12.1.