Safari ya Kinyago United hadi ubingwa wa Odi Bet mtaani
Na JOHN KIMWERE
KINYAGO United imedhihirishia mahasimu wao Biafra FC ingali moto wa kuotea moto baada ya kuwanyoroshwa na kubeba taji la Odi Bet mtaani katika fainali iliyosakatiwa Uwanja wa Desert Kamukunji, Nairobi.
Kinyango ya kocha Anthony Maina ilituzwa bingwa wa kipute hicho ilipolaza Biafra FC mabao 2-1 kupitia mipigo ya matatu baada ya kutoka nguvu sawa magoli 2-2.
Timu zote zilishuka dimbani huku wafuasi wazo wakiwa tayari kushuhudia mchezo huo wa debi. Biafra iliyojumuisha wachezaji kadhaa ambao hushiriki kipute cha Betika Supa Ligi ya Taifa (BNSL) ilianza patashika hiyo kwa kasi ambapo ilifunga bao la kwanza ndani ya dakika tano za kwanza.
Mchezo huo ulishuhudia ushindani wa kufa mtu huku pande zote zikishusha makombora makali makali sio mzaha.
ALINOGESHA
Katika muda wa kawaida Keith imbali na Samuel Ndonye waliofungia Kinyago bao moja kila mmoja. Kwa jumla mnyakaji Alex Nzuki alinogesha timu hiyo kwa kuokoa mikwaju miwili na kubeba Kinyago kunyakua taji hilo.
”Dah! Bila wazi kwanza vijana wangu wamenyorosha wapinzani wapinzani wetu na kutuzwa kombe la Odi bet. Hongera kwa kikosi changu haikuwa mteremko bali kazi zito waliotekeleza tangia mwanzo hadi mwisho,” kocha wa Kinyago alisema na kuongeza kuwa waliibuka mabingwa licha ya wapinzani wao kuwapuuza.
Kwa kuonyesha soka la kuvutia alitoa shukran zake wachezaji wote kwa jumla na kusema uwepo wao ulisaidia ufanisi huo.
MICHAEL OLUNGA
”Tunafuraha kutaja kwamba tumepania kutembea katika mitaa yote huku tukiandaa mechi za mchezo wa soka ili vijana kupata nafasi kuonyesha talanta zao. La muhimu wachezaji wa timu zote zitakaokuwa zinashiriki watakuwa wakipokea jezi,” alisema meneja wa mauzo wa Odi bet, Aggrey Sayi na kutoa mwito kwa wachezaji chipukizi kutia bidii kukuza talanta zao maana wao ndio Michael Olunga na Victor Wanyama wa kesho.
SAFARI
Kwenye mechi za robo fainali, Kinyago ilivuna ufanisi wa mabao 2-1 dhidi ya Calif United baada ya kutoka nguvu sawa bao 1-1. Katika nusu fainali wachezaji hao walitwaa ushindi sawa na huo baada ya kuagana magoli 2-2. Kwenye utangulizi Kinyango ilishinda mabao 2-1 mbele ya Wenyeji Youth.
Kinyago ilijumuisha: Dominic Waithaka, Keith Imbali, Stephen Mooley, Julius Kyalo, Patrick Gitonga, Henry Thierry, Jahson Wakachala, Ian Ochieng, Fortune Omondi, James Mwawasi (nahodha), Abednego Wawire, Alex Nzuki (kipa) na Samuel Ndonye.