• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Sammy Nyokaye aelekeza macho kwa kivumbi cha Rock City Half Marathon mjini Mwanza, Tanzania

Sammy Nyokaye aelekeza macho kwa kivumbi cha Rock City Half Marathon mjini Mwanza, Tanzania

Na CHRIS ADUNGO

LICHA ya kutoshiriki mashindano yoyote kwa muda wa miezi saba, mwanariadha Sammy Nyokaye anapigiwa upatu wa kuibuka mshindi wa mbio za Rock City Half Marathon mjini Mwanza, Tanzania mnamo Novemba 29, 2020.

Bingwa huyo wa zamani wa Mully Half Marathon, alitazamiwa kunogesha mbio za kilomita 42 za Manchester na Ottawa marathon kabla ya mitimko hiyo kuahirishwa kwa sababu ya janga la corona mnamo Aprili.

“Nimeshiriki mazoez ya kutosha na ninajihisi kuwa katika hali shwari itakayoniwezesha kutamba kwenye mashindano haya nchini Tanzania,” akasema Nyokaye.

Mnamo 2015, Nyokaye aliambulia nafasi ya pili kwenye Nusu Marathon ya Rock City baada ya kutupwa hadi nafasi ya nne kwenye mbio hizo mnamo 2014.

“Riadha ndicho kitega-uchumi changu kikuu. Japo sijashiriki mbio zozote tangu Aprili, nimekuwa nikijiandaa kwa matarajio ya kutifua kivumbi kwenye chochote. Nafuu zaidi ni kwamba nimewahi kukimbia mjini Mwanza na naelewa jinsi ya kujifua ipasavyo kwa kivumbi hicho. Nitakuwa na kila sababu ya kuibuka mshindi,” akaongeza.

Nyokaye alipata umaarufu mnamo 2017 baada ya kutawala mbio za Mully Half Marathon. Ni mwaka uo huo ambapo aliambulia nafasi ya nne kwenye mbio za kilomita 10 za Samuel Wanjiru Discovery kabla ya kuridhika na nafasi ya tano kwenye Madoka Half Marathon.

Anajivunia tajriba pevu na uzoefu mkubwa kwenye ulingo wa riadha hasa ikizingatiwa kwamba amewahi kuweka kasi kwenye marathon za haiba kubwa ikiwemo Barcelona Marathon aliyoikamilisha kwa muda wa saa 2:14:50.

You can share this post!

Mitihani ya majaribio yaanza

Dalili za ugonjwa wa kisukari