Schalke 04 yaikaribisha Manchester City
BERLIN, Ujerumani
MANCHESTER City watazuru jijini Gelsenkirchen leo Jumatano usiku kupambana na wenyeji Schalke 04 katika mechi ya duru ya kwanza ya gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), hatua ya 16-bora.
Vijana hao wa kocha Pep Guardiola walipoteza mechi moja pekee katika Kundi G na kumaliza katika nafasi ya kwanza.
Klabu hii imekuwa katika kiwango kizuri tangu mwezi Desemba ambapo imeshinda mechi 11 kati ya 12 katika mashindano mbalimbali, huku ikifunga jumla ya mabao 46.
Schalke kwa upande wao, wanajivunia wachezaji kadhaa walio na ujuzi wa mechi kubwa, na pia wamekuwa na rekodi nzuri ugani Veltina Arena ambako ndiko mechi hiyo itachezewa.
Walimaliza ligi katika nafasi ya pili, nyuma ya Bayern Munich, lakini msimu huu hali imekuwa ngumu kiasi cha kushindwa kuondoka katika eneo la hatari.
Katika kiwango cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), klabu hiyo maarufu kama Die Konigsblauen ilimaliza ya pili, na pia sawa na City, walimaliza mechi ya makundi kwa kupoteza mechi moja pekee.
City wataingia uwanjani siku chache baada ya kuicharaza Newport County 4-1 wakati ambapo Schalke waliagana 0-0 na Freiburg kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani.
Wenyeji chini ya kocha Domenico Tedesco watacheza mechi ya leo bila nyota kadhaa kutokana na majeraha, lakini Kinda Rabbi Matondo atapata fursa ya kucheza dhidi ya klabu yake ya zamani, Manchester City kabla ya kuyoyomea Bundesliga mapema mwaka 2019.
Kadhalika, itakuwa fursa nzuri kwa mlinzi Matija Nasralic kucheza dhidi ya Manchester City, timu yake ya zamani.
Sebastian Rudy ambaye majuzi alihusishwa na mpango wa kujiunga na mabingwa hao wa EPL pia atakuwa kikosini kusaidia Schalke kupata matokeo mema kwenye mechi hii ya mkondo wa kwanza.
Wachezaji wengine wanaotarajiwa kupewa nafasi kikosini ni pamoja na Amine Harit na Weston McKennie.
Suart Serdar aliyeonyeshwa kadi nyekundu mwishoni mwa wiki hatakuwa kikosini, pamoja na Omar Mascarell atakayesubiri hadi mkondo wa pili kutokana na kadi alioonyeshwa katika mechi ya awali.
Benjamin Stambouli na Rudy watakosa kucheza mechi ya marudiano iwapo wataonyeshwa kadi ya pili ya manjaoi katika mechi hiyo.
Kwa upnade mwingine, Nicolas Otamendi, Sergio Aguero na Fermandinho watakosa kucheza mkondo wa pili iwapo wataonyeshwa kadi za njano.
Benjamin Mendy na Vincent Kompany wanasumbuliwa na majeraha na huenda wasijumuishwe kikosini.
Danilo au Oleksandr, mmoja wao ataanza kama beki wa kushoto katika kikosi hiki cha kocha Pep Guardiola.
Huenda Leroy Sane akaanza kama mchezaji wa akiba dhidi ya klabu hiyo yake ya zamani (Schalke).