Michezo

SEMA NAMI: Kipchoge aomba kukutana na Obama

October 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

BINADAMU wa kwanza kukamilisha mbio za kilomita 42 chini ya saa mbili, Eliud Kipchoge sasa anataka uungwaji mkono kutoka kwa Rais Mstaafu wa Amerika Barack Obama katika juhudi zake za kueneza ukimbiaji kote duniani.

Wito wake kwa Rais huyo wa zamani wa Amerika ulitokana na Obama kumpongeza kwa kuwa mtu wa kwanza kupata ufanisi huo katika mbio maalum za INEOS 1:59 Challenge ambazo ziliandaliwa Jumapili na Mkenya huyo akakamilisha kwa saa 1:59:40 jijini Vienna nchini Austria.

Obama, ambaye ana asili ya Kenya, aliandika kwenye mtandao wake wa Twitter siku ya Jumapili akisema, “Jumamosi, mwanariadha Eliud Kipchoge aliingia katika daftari la kumbukumbu kwa kuwa wa kwanza kabisa kukimbia marathon kwa muda wa chini ya saa mbili. Jumapili mjini Chicago, Brigid Kosgei aliweka rekodi mpya ya dunia ya wanawake. Walipata mafanikio makubwa wenyewe. Wao ni mifano mizuri sana ya uwezo wa binadamu kuvumilia — endeleeni kuweka viwango vya juu.”

Kipchoge, ambaye ni bingwa wa Olimpiki na marathon za kifahari za London (2015, 2016, 2018 na 2019), Berlin (2015, 2017 na 2018) na Chicago (2014), alifurahia kupokea ujumbe huo kutoka kwa rais huyo mustaafu wa 44 wa Marekani.

Hapo jana, Kipchoge alijibu Rais Obama, “Bw Obama, asante sana kwa ujumbe wako spesheli. Maishani, tunatumai kuwapa wengine motisha. Asante kwa kunipa motisha.””

Kipchoge kisha aliomba Rais Obama akutane naye. Alisema, “Itakuwa heshima kubwa sana kwangu iwapo utaandaa kikao nami. Tukutane tujadiliane jinsi tunaweza kufanya dunia nzima ichukulie kwa uzito ukimbiaji. Dunia ya ukimbiaji ni dunia ya amani. Hakuna lisilowezekana.”

Kuwekewa kasi

Mkimbiaji huyu, ambaye atasherehekea kufikisha umri wake miaka 35 mnamo Novemba 5 aliwekewa kasi na watimkaji 41 katika mbio hizo zilizodhaminiwa na bwanyenye Mwingereza Jim Ratcliffe.

Hili lilikuwa jaribio la pili la Kipchoge kukamilisha umbali huo chini ya muda wa saa mbili baada ya kutimka mbio za Nike Breaking2 mjini Monza nchini Italia kwa saa 2:00:25 mwaka 2017.

Kipchoge, ambaye anashikilia rekodi rasmi ya marathon ya saa 2:01:39 aliyoweka aliposhinda Berlin Marathon mwaka jana, alimiminiwa sifa kutoka pembe zote za dunia kwa ufanisi wake mjini Vienna.

Baadhi ya viongozi waliotaka kuhusishwa na mafanikio ya Kipchoge ni Marais Uhuru Kenyatta na Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Naibu Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM Raila Odinga miongoni mwa wengine.

Kupitia mbio hizo maalum, Kipchoge alitaka kuonyesha ulimwengu kuwa hakuna kitu kinachoweza kumzuia binadamu kutimiza ndoto yake mradi tu atie bidii na kujiamini.

Kosgei alivunja rekodi ya dunia ya marathon ya wanawake ya mbio za mseto ya saa 2:15:25 iliyoshikiliwa na Mwingereza Paul Radcliffe ya London Marathon mwaka 2003.

Mkenya huyu alihifadhi taji la Chicago Marathon kwa saa 2:14:04 siku ya Jumapili.