Michezo

Setien kuishtaki Barca

September 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

KOCHA wa zamani wa Barcelona, Quique Setien na waliokuwa wasaidizi wake watatu kambini mwa miamba hao wa soka ya Uhispania, wamefichua mpango wa kushtaki kikosi hicho kwa kutotii masharti ya kandarasi zao baada ya kupigwa kalamu mnamo Agosti 2020.

Kwa mujibu wa Setien na wenzake, Barcelona iliwapokeza notisi ya kutamatisha kandarasi zao mnamo Septemba 16 licha ya miamba hao wa soka duniani kuwatimua Agosti 17.

Aidha, Setien alisema kwamba hakuna yeyote katika iliyokuwa benchi yake ya kiufundi uwanjani Camp Nou alikuwa amelipwa fidia yoyote na barua ambayo yeye na wenzake walipokezwa na Barcelona mnamo Septemba 16 haikutaja mpango wowote wa kulipwa kwao.

“Barua kutoka kwa Barcelona inaashiria kwamba kikosi hicho hakina mpango wowote wa kutimiza masharti ya mikataba tuliyokuwa nayo tangu Januari 14, 2020,” akasema Setien.

Barcelona walimfuta kazi Setien siku tatu baada ya kikosi hicho kudhalilishwa kwa kichapo cha 8-2 kutoka kwa Bayern Munich ya Ujerumani kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) jijini Lisbon, Ureno.

Kutimuliwa kwake kulimpisha mkufunzi Ronald Koeman aliyewahi kuvalia jezi za Barcelona kati ya 1989 na 1995. Koeman aliajiriwa baada ya kushawishika kubanduka kambini mwa timu ya taifa ya Uholanzi.

Setien ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Real Betis, aliajiriwa na Barcelona mnamo Januari 2020 na alikuwa amesimamia jumla ya mechi 25 za Barcelona hadi kutimuliwa kwake.

Chini ya Setien, 61, Barcelona walikamilisha kampeni zao za msimu huu bila taji lolote kwa mara ya kwanza tangu 2008. Barcelona walikamilisha msimu huu kwenye La Liga katika nafasi ya pili kwa alama tano nyuma ya mabingwa Real Madrid.

Kichapo ambacho Barcelona walipokezwa na Bayern kwenye UEFA kilikuwa cha nne katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ambayo iliwabandua kwenye robo-fainali za kipute hicho cha bara Ulaya.

Setien alimrithi kocha Ernesto Valverde uwanjani Camp Nou mwanzoni mwa 2020.

Baada ya kumtimua Setien, Barcelona walisema: “Haya ndiyo maamuzi ya kwanza kati ya mengi ambayo tunalenga kuchukua katika juhudi za kukisuka upya kikosi chetu.”

Barcelona pia walimtangaza Ramon Planes kuwa mkurugenzi mpya wa kiufundi kambini mwao. Planes alikuwa msaidizi wa Eric Abidal aliyetimuliwa na Barcelona akiwa mkurugenzi wa spoti.

Koeman alianza safari yake ya ukufunzi akiwa msaidizi wa Guus Hiddink katika timu ya taiga ya Uholanzi na kwa pamoja, wakakiongoza kikosi hicho kwenye fainali za Kombe la Dunia mnamo 1998. Baada ya hapo aliaminiwa kuwa kocha msaidizi wa Louis van Gaal kambini mwa Barcelona kati ya 1998 na 2000.

Alirejea baadaye nchini Uholanzi alikodhibiti mikoba ya klabu za Ajax na PSV. Akiwa kocha wa Valencia alikohudumu kwa kipindi kifupi mnamo 2007, Koeman aliongoza kikosi hicho kutwaa ubingwa wa Copa del Rey. Alitimuliwa baada ya kikosi hicho kukamilisha msimu huo wa La Liga katika nafasi ya 17 kwa alama mbili pekee nje ya mduara wa klabu zilizoshuka daraja.

Baada ya kuhudumu pia kambini mwa AZ Alkmaar na Feyenoord, Koeman alipokezwa mikoba ya Southampton mnamo 2014 alikowasaidia kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza katika nafasi ya sita na saba zilizowakatia tiketi ya kushiriki kivumbi cha Europa League.

Everton walimsajili mnamo 2017 ila akahuhumu uwanjani Goodison Park kwa miezi 16 pekee kabla ya kufutwa na kikosi hicho kilichoambulia nafasi ya 17.

Licha ya matokeo duni yaliyosajiliwa na Everton chini ya ukufunzi wa Koeman, kocha huyo aliajiriwa na timu ya taifa ya Uholanzi mnamo Februari 2018. Uholanzi walihitaji ufufuo mkubwa baada ya kushindwa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2018 nchini Urusi.

Chini ya Koeman, Uholanzi walitinga fainali ya Uefa Nations League mnamo 2019 na akawasaidia kufuzu kwa fainali za Euro 2020.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO