Shabana FC kusajili wanachama 10,000 wa kudumu
Na CHRIS ADUNGO
KIKOSI cha Shabana FC kinachoshiriki Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL), kimezindua mpango wa kusajili wanachama wapya 10,000 wa kudumu.
Rais wa kikosi hicho, Jared Nivaton amesema wote wanaopania kujisajili na kikosi hicho wanatarajiwa kulipa ada ya Sh1,000.
“Baada ya kushauriana na washikadau mbalimbali, tumeafikiana kuanza mchakato wa kusajili wanachama zaidi kutoka sehemu mbalimbali za nchi,” akasema Nivaton.
“Baada ya shughuli ya usajili, tutawataka wanachama wote wajiweke kwenye kategoria za kulipia ada ya uanachama ama kila mwezi au kila mwaka. Fedha hizi zitawezesha kikosi kujiendesha na kufanikisha shughuli za mara kwa mara,” akaongeza kinara huyo.
Shabana FC kwa sasa wanapania pia kufufua matawi yao ya Kisii, Nyamira, Kisumu, Kericho, Nakuru, Nairobi na Mombasa na kupanua uanachama wa kikosi.
“Nahimiza mashabiki wa Shabana FC wajisajili kwa wingi ili shughuli za kuendesha klabu ziwe nyepesi,” akasema Nivaton kwa kusisitiza kwamba kikosi chake kwa sasa kinajiandaa kurejelea mazoezi kwa minajili ya kampeni za muhula ujao.
“Hii ni hatua kubwa katika makuzi na maendeleo ya klabu ya Shabana FC. Wingi wa wanachama wa klabu ni ishara ya kuimarika kwa uthabiti wa kikosi,” akasema Mwenyekiti mpya wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) katika Kaunti ya Kisii, Jezreel Mbegera.