Shabana yaonyesha ubabe kwa kuzaba KCB na kupaa hadi nambari 2 ligi kuu
SHABANA jana walionyesha uzito wao kwa kulemea KCB 3-1 kwenye mechi ya Ligi Kuu (KPL) kwenye uwanja wa MISC Kasarani.
Mabao ya Glamour Boys wa Tore Bobe yalifungwa na Kevin Omundi, Ezekiah Omuri na Humprey Obina huku Kelvin Etemesi akifungia KCB bao la kufutia machozi.
Shabana walipata ushindi huo siku ambayo Kocha wao Peter Okidi alitajwa Kocha Bora wa Novemba.
Ushindi huo ulikuja baada ya Shabana kubambwa sare tasa na Mara Sugar katikati mwa wiki ugani Gusii.
Kwenye kikosi kilichoanza aliwapa nafasi Ezekiah Omuri na David Odoyo na kuwaweka kwenye benchi Douglas Mokaya na Victor Omondi.
Kwa upande wake kocha wa KCB, Robert Matano, alimpa nafasi Matthias Isogol kwa sababu Jack Onganya anaendelea kuuguza majeraha.
Josphat Andafu aliingia pahala pa Nashon Wekesa.
Dakika ya 14 Humprey Obina aliupiga mpira wa ikabu ambao uliangukia Wycliffe Omondi na mshambulizi huyo akaachilia fataki.
Hata hivyo, kipa wa KCB Arnold Monozobo aliupangua mpira huo na ukaangukia Kevin Omondi ambaye aliujaza wavuni.
Obina aliongeza la pili kwa KCB akifunga kupitia mpira wa ikabu.
Dakika chache baada ya kipindi cha pili kuanza, Etemesi alifungia KCB na kufikisha idadi ya mabao aliyofunga ligini hadi sasa kuwa mabao saba.
Ndiye anaongoza orodha ya wafungaji kwenye KPL hadi sasa.
Maji yalizidi unga wa KCB baada ya Ezekiel Omuri ambaye ni nyota wa Harambee Stars U-20 kufungia Shabana bao la tatu.
Ushindi wa Shabana una maana kuwa wameshinda mechi tatu mfululizo dhidi ya KCB.
Tore Bobe sasa wapo nafasi ya pili na alama 23 baada ya kusakata mechi 14. Wako na alama sawa na viongozi Gor Mahia ambao wamecheza mechi 12 na watavaana na Nairobi United leo.
Nayo KCB, ambayo ingetua kileleni mwa jedwali la KPL iwapo ingezoa ushindi, sasa imesalia katika nafasi ya tatu na alama 22.
Kuhusu mechi ya Gor kocha wa Nairobi United Nicholas Muyoti, alisema shabaha yao ni kuzoa alama zote tatu.
“Gor ni timu ambayo ina wachezaji wazoefu na kati ya timu bora msimu huu. Kwa hivyo, lazima tujitume tukitaka alama tatu,” akasema Muyoti.
Mara ya mwisho ambapo timu hizo zilikutana ni msimu uliopita ambapo zilicheza kwenye fainali ya Kombe la Mozzart.
Naibois walishinda mechi hiyo kupitia mkwaju wa penalti baada ya timu hizo kuagana sare tasa katika muda wa kawaida.