• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
Sharks yachemkia Asante Kotoko kudai imepata mapokeo duni

Sharks yachemkia Asante Kotoko kudai imepata mapokeo duni

Na GEOFFREY ANENE

SAA chache kabla ya Kariobangi Sharks kuvaana na wageni wake Asante Kotoko katika mechi ya mechi wa kwanza ya raundi ya kwanza ya Kombe la Mashirikisho jijini Nairobi, wenyeji wamepuzilia mbali madai kwamba wamewapa Waghana hao mapokezi mabaya.

Katika taarifa kwenye mtandao wake wa Twitter, mabingwa wa SportPesa Shield, Sharks, wamesema, “Inasikitisha sana kwamba wapinzani wetu wameamua kutumia uongo kutuharibia sifa kwamba tumewanyanyasa. Tungependa kuwafahamisha kwamba tumefuata sheria za mashindano haya jinsi Shirikisho la Soka la Bara Afrika (CAF) inasema na tutaendelea kuzifuata.”

Sharks imelalamika kwamba hata umma unafahamu kwamba Kotoko ilikataa kufichulia klabu hiyo mipango yake na “ilipowasili tu katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi ilianza kuitisha vitu ambavyo viko nje ya sheria za CAF. Vitu kama hivi havifai katika soka ya wakati huu.”

Wakenya hao wameongeza, “Wapinzani wetu wakome kutumia uvumi kama huo kuwa sababu ya kufanya vitendo ambavyo vinakosa maadili na ambavyo inaonekana wanapanga kufanya tutakapozuru mji wa Kumasi kwa mechi ya marudiano.”

“Mwisho, ikiwa wanahisi tumewatendea visivyo, basi waandike barua rasmi ya malamishi kwa CAF. Tuangazie soka na tuwache vijisababu,” Sharks imeandika saa chache tu baada ya kukamilisha mazoezi yake ya mwisho uwanjani Kasarani hapo Ijumaa.

Mabingwa mara 23 wa Ghana, Asante Kotoko hawajajibu Sharks. Hata hivyo, wameandika kwenye mtandao wao wa Twitter kwamba wanaelekea Kasarani kufanya mazoezi. “Tumefunga safari yetu kuelekea uwanjani Kasarani kwa mazoezi ya kabla ya siku ya mechi kulingana na sheria za CAF.”

Sharks inashiriki mashindano ya Afrika kwa mara ya kwanza katika historia yake. Kotoko inafahamu mashindano ya Afrika ndani-nje. Imeshiriki mashindano mbalimbali ya Afrika kwa mwaka 36 yakiwemo Klabu Bingwa.

Timu hizi mbili zilifika katika raundi ya kwanza kupitia njia tofauti. Sharks ilichapa Arta Solar7 ya Djibouti 6-1 jijini Nairobi na kushinda mechi ya marudiano 3-0 ugenini. Kotoko ilinyakua tiketi bila kupiga mpira baada ya Cameroon kuchelewa kutangaza mwakilishi wake kufikia siku ya mwisho ya kufanya hivyo Oktoba 15, 2018.

  • Tags

You can share this post!

Referenda yaja, Uhuru adokezea Wakenya

Kenya nje ya tuzo za wakali wa soka Bara Afrika 2018

adminleo