She-Flames ya Malawi yawasili kumenyana na Harambee Starlets mechi ya kuingia Olimpiki
Na GEOFFREY ANENE
TIMU ya taifa ya soka ya wanawake ya Malawi almaarufu She-Flames imewasili nchini Kenya tayari kwa mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya kufuzu kushiriki Olimpiki mwaka 2020 dhidi ya Harambee Starlets itakayosakatwa Jumapili.
Warembo wa kocha Abel Mkandawire walitua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyataa jijini Nairobi mnamo saa tano usiku Ijumaa.
Baada ya kuwasili, She-Flames ilielekea mjini Machakos ambako mechi hiyo itachezewa na kupata makao katika hoteli ya kifahari ya Gelian.
Timu hiyo, ambayo ilichapa Starlets 3-2 katika mechi ya mkondo wa kwanza jijini Blantyre mnamo Agosti 28, inatarajiwa kufanya mazoezi mepesi Jumamosi asubuhi kisha baadaye iwe na mazoezi makali jioni uwanjani Kenyatta.
Kutokana na ushindi katika mechi ya mkondo wa kwanza, She-Flames iko mguu mmoja ndani ya raundi ya tatu. Inahitaji sare ya aina yoyote kusonga mbele tofauti na Starlets ambayo lazima ishinde ili isalie mashindanoni.
Mechi hii itasakatwa katika uwanja bila mashabiki kwa sababu uwanja wa Kenyatta haujaidhinishwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kuandaa mechi za kimataifa.
Uwanja wa Kasarani, ambao umekuwa ukutumiwa kwa mechi za kimataifa, umekuwa ukitumiwa kwa michezo ya Maafisa wa Polisi kutoka eneo la Afrika Mashariki na Kati (EAPCCO).
Harambee Starlets inafundishwa na kocha David Ouma.