Shujaa kupigania tiketi ya Olimpiki kwenye Kombe la Afrika
Na GEOFFREY ANENE
KENYA iko katika orodha ya mataifa 14 yatakayowania tiketi ya kushiriki raga ya wachezaji saba kila upande kwenye Olimpiki mwaka 2020 katika Kombe la Bara Afrika la wanaume litakaloandaliwa mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini mnamo Novemba 8-9, 2019.
Shirikisho la Raga la Afrika (Rugby Afrique) limetangaza kwamba mabingwa hawa wa Afrika mwaka 2004, 2008, 2013 na 2015 watapigania tiketi hiyo moja dhidi ya Zimbabwe, Uganda, Madagascar, Zambia, Tunisia, Senegal, Morocco, Namibia, Ghana, Botswana, Mauritius, Ivory Coast na Nigeria.
Limeongeza: “Tunasubiri matokeo ya Raga ya Dunia ya msimu 2018-2019 kufahamu kama Afrika Kusini itafuzu kwa kumaliza raga hiyo katika nafasi nne za kwanza ama itajumuishwa katika Kombe la Afrika isipofuzu kupitia Raga ya Dunia. Vilevile, huenda Burkina Faso ikapata nafasi ya kuwania ubingwa wa Afrika.”
Zimbabwe ni mabingwa wa Afrika mwaka 2000, 2012, na 2018 ilipopiga Kenya katika fainali 17-5.
Kenya iliponea chupuchupu kukosa makala ya kwanza ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Olimpiki mwaka 2016 pale ilipohitaji mguso wa ushindi sekunde chache kabla ya kipenga cha mwisho kulia kutoka kwa Dennis Ombachi kuzima Zimbabwe 19-17 na kujikatia tiketi ya kuelekea Rio de Janeiro nchini Brazil.
Bara Afrika iliwakilishwa na Kenya na Afrika Kusini katika Olimpiki mwaka 2016. Afrika Kusini ilifuzu kwa kumaliza Raga ya Dunia ya msimu 2014-2015 katika nafasi ya pili.
Kenya ilifanya vibaya katika Olimpiki ilipochapwa na Uingereza (31-7), New Zealand (28-5) na Japan (31-7) katika mechi za makundi, ikalemewa na Uhispania 14-12 katika mechi ya kuorodheshwa nafasi ya tisa hadi 12 kabla ya kuponea kumaliza mkiani kwa kubwaga 24-0 katika mechi ya kutafuta nambari 11 na 12 (mwisho).
Kwa sasa, Afrika Kusini inashikilia nafasi ya nne katika Raga ya Dunia ya msimu 2018-2019 kwa alama 121 zikisalia duru za London nchini Uingereza mnamo Mei 25-26 na Paris nchini Ufaransa mnamo Julai 1-2.
Kenya ni ya 13 kwa alama 26.