Michezo

Sierra Leone yaapa kuipa Ghana kipigo cha pili

October 4th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

SIERRA Leone imeonya Ghana ijiandae kwa kichapo cha pili mfululizo baada ya kulazwa na Harambee Stars zitakapokutana katika mechi nyingine ya Kundi F ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) hapo Oktoba 11, 2018.

Leone Stars ya Sierra Leone na Black Stars ya Ghana zilipepetwa ugenini 1-0 na Ethiopia na Kenya mnamo Septemba 8 na Septemba 9, mtawalia. Ina maana kwamba zitaingia mchuano wao wa tatu, ambao utasakatwa mjini Kumasi, zikiwa kama simba aliyejeruhiwa.

“Tunakuja kushangaza Ghana katika ardhi yao wala si kutalii ama kujiburudisha mjini Kumasi,” Mkurugenzi wa Mashindano kwenye Shirikisho la Soka la Sierra Leone (SLFA) Sorie Ibrahim amenukuliwa na tovuti ya Ghana Soccernet aliambia redio ya Oyerepa FM.

“Tutawapa Ghana ushindani kwao. Kama wanadhani watalemea Sierra Leone, basi wafikirie tena.” Ghana inaongoza kundi hili kwa alama tatu baada ya kucharaza Ethiopia 5-0 mjini Kumasi mnamo Juni mwaka 2017.

Kenya ni ya pili kwa alama tatu kutokana na ushindi wake wa bao 1-0 dhidi ya Ghana. Nambari tatu Sierra Leone ina alama tatu ilizopata kwa kulima Kenya 2-1 Juni mwaka 2017. Ethiopia iko mkiani kwa alama tatu ilizovuna kwa kuchapa Sierra Leone nchini Ethiopia mwezi Septemba mwaka huu wa 2018.

Kundi hili ni wazi baada ya timu zote kushinda mechi moja na kupoteza moja. Kenya inajiandaa kumenyana na Ethiopia mjini Bahir Dar mnamo Oktoba 10 na kurudiana na majirani hawa wake jijini Nairobi mnamo Oktoba 14.

Timu mbili za kwanza katika kundi hili zitaingia AFCON mwaka 2019.