• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Sierra Leone yatuma nyuma kupata sare ya 4-4 dhidi ya Super Eagles

Sierra Leone yatuma nyuma kupata sare ya 4-4 dhidi ya Super Eagles

Na MASHIRIKA

SIERRA Leone walitoka nyuma kwa mabao manne bila jibu na kulazimishia Super Eagles ya Nigeria sare ya 4-4 katika mechi ya kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Afrika (AFCON) mnamo Novemba13 jijini Benin City, Edo State, Nigeria.

Gozi hilo lilikuwa mojawapo ya mechi sita za makundi zilizopigwa Ijumaa kwa minajili ya fainali za AFCON zitakazoandaliwa nchini Cameroon mnamo 2022.

Katika michuano mingine ya Novemba 13, sajili mpya wa Chelsea, Hakim Ziyech alifungia Morocco mabao mawili na kuhakisha kwamba wanasajili ushindi wa nyumbani sawa na Mali, Niger na Afrika Kusini.

Nigeria waliingia kwenye mechi hiyo wakilenga kusajili ushindi wa tatu mfululizo katika Kundi L. Fowadi wa Everton, Alex Iwobi alifunga mabao mawili na mengine kupachikwa wavuni na Victor Osimhen wa Napoli na Samuel Chukwueze wa Villarreal chini ya dakika 30 za kipindi cha kwanza.

Hata hivyo, Sierra Leone walirejea mchezoni kupitia kwa Kwame Quee mwishoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya Alhaji Kamara kufanya mambo kuwa 4-2 katika dakika ya 72. Mustapha Bundu alifungia Sierra Leone goli la tatu kunako dakika ya 80 kabla ya Kamara kusawazisha sekunde chake kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupuliwa.

Licha ya sare hiyo, Nigeria wanasalia kileleni mwa kundi lao kwa alama saba, mbili zaidi kuliko Sierra Leone wanaoshikilia nafasi ya tatu. Benin walijibwaga jana ugani kuvaana na Lesotho katika mchuano mwingine wa Kundi L.

Mabao mawili kutoka kwa Ziyech yalisaidia Morocco kupepeta Central African Republic (CAR) 4-1 na kupaa hadi kileleni mwa Kundi E. Magoli mengine ya Morocco yalifumwa wavuni na Achraf Hakimi na Zakaria Aboukhlal aliyekuwa wakiwajibishwa katika timu ya taifa kwa mara ya kwanza. CAR walifutiwa machozi Louis Mafouta. Morocco kwa sasa wanaselelea kileleni mwa kundi lao kwa alama saba, mbili zaidi kuliko Mauritania ambao ni wa pili.

Afrika Kusini walihitaji penalti ili kusajili ushindi wa 2-0 uliowaepushia kuepuka aibua ya kuangushwa na Sao Tome Principe, taifa dogo lililo na raia 200,000 pekee ambalo linashikilia nafasi ya 182 kwenye orodha ya kimataifa ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Percy Tau aliwafungulia Afrika Kusini ukurasa wa mabao kunako dakika ya 55 kabla ya Bongani Zungu kuongeza la pili jijini Durban. Afrika Kusini kwa sasa ni wa pili kwenye Kundi C kwa alama sita, tatu nyuma ya viongozi Ghana.

Tunisia wanajivunia alama tisa kutokana na mechi tatu za Kundi J baada ya kufunga Tanzania 1-0 jijini Tunis. Bao hilo lilifumwa wavuni na Youssef Msakni kupitia penalti.

Mali waliungana na Guinea kileleni mwa Kundi A baada ya kusajili ushindi wa 1-0 dhidi ya Namibia jijini Bamako. Mfungaji wa bao hilo la pekee alikuwa tineja El Bilal Toure katika dakika ya 38.

Kwingineko, Niger waliwapokeza Ethiopia kichapo cha 1-0 katika mechi ya Kundi K jijini Niamey. Bao hilo lilijazwa kimiani na Youssef Oumarou kupitia penalti. Niger na Ethiopia kwa sasa wanajivunia alama tatu kila mmoja, tatu nyuma ya viongozi Ivory Coast na Madagascar.

MATOKEO YA AFCON:

Niger 1-0 Ethiopia (Kundi K)

Nigeria 4-4 Sierra Leone (Kundi L)

Mali 1-0 Namibia (Kundi A)

Morocco 4-1 CAR (Kundi E)

Afrika Kusini 2-0 Sao Tome & Principe (Kundi C)

Tunisia 1-0 Tanzania (Kundi J)

TAFSIRI: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

TANZIA: Mwendwa na Nyamweya wamwomboleza Rais wa zamani wa...

Timu zaanza kujiandaa kwa Ligi Kuu ya Wanawake msimu huu