• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
SIKATI TAMAA: Eriksen akosa kujiunga na Real Madrid

SIKATI TAMAA: Eriksen akosa kujiunga na Real Madrid

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

CHRISTIAN Eriksen amesema kwamba hakuwa na uwezo wa kuamua hatima yake katika kipindi kilichopita cha uhamisho wa wachezaji baada ya kukosa kujiunga na Real Madrid ya Uhispania.

Mnamo Juni 2019, kiungo huiyo wa Tottenham Hotspur alisema kwamba alikuwa tayari kuondoka Uingereza na kutafuta hifadhi mpya kwingineko.

Ingawa hivyo, alijipata bado akiwa mchezaji wa Spurs mwishoni mwa dirisha la uhamisho Jumatatu iliyopita.

Kiungo huyo anayejiandaa na kikosi cha timu ya Denmark inayojiandaa kucheza na timu za Gibraltar pamoja na Georgia leo Alhamisi na Jumapili, alisema: “Ingekuwa bora kama ningekuwa na uwezo wa kuiamulia, lakini sasa uwezo huo haupo mikononi mwangu. Hata hivyo, sijakata tamaa, nitasubiri kuona kitakachotokea. Mpirani, chochote chaweza kutokea.”

Eriksen alianza katika mechi zote nne za Spurs msimu huu, lakini anasisitiza ingekuwa bora kama shughuli zote za uhamisho barani Ulaya zingemalizika kwa wakati mmoja.

“Ninaamini klabu nyingi barani Ulaya zingefurahia iwapo msimu wa uhamisho ungemalizika kwa wakati mmoja,” alisema. “Mabadiliko ya ghafla yaliyotokea yaliwapoa makocha kazi ngumu ya kutojua wachezaji watakaokuwa nao kwa msimu mpya. Ningefurahia kucheza mechi zote kuanzia mwanzo, lakini lazima kocha aamue.”

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 ambaye amekuwa na Tottenham tangu 2013, alisema uvumi ulioenea katika vyombo vya habari kuhusu hali yake ya baadaye kamwe haukufuruka akili yake.

“Kawaida yangu sisomi zaidi kuhusu habari zinazoandikwa magazetini kunihusu. Nimezoea kusoma mengi kuhusu madai kwa miaka mingi. Mengi yameandika, hata wengine wakaanza kudai nilionekana Madrid nikitafuta nyumba ya kuishi, lakini hayo yote hayakunivuruga. Nilikuwa huko kujifurahisha tu wakati wa likizo. Tulizuru barani Asia lakini sikuona habari za aina hiyo. Ni vyema kuzuru sehemu nyingine za dunia.”

Wakati huohuo, klabu ya Manchester United imezidisha juhudi zake za kutafuta kipa wa kurithi David de Gea ambaye anapanga kuondoka mapema mwaka 2020.

Mlinda lango huyo raia wa Uhispania amebakisha mwaka mmoja kwenye mkataba wake ambao utafika ukingoni mwa msimu huu.

Usajili

Kipa huyo mwenye umri wa miaka 28 alikataa kusaini mkataba mpya kuendelea kuichezea Manchester na sasa anapanga kuhamia PSG wakati wa dirisha dogo la usajili Januari mwakani.

Katika juhudi hizo kubwa za kutafuta mtu wa kumrithi, Manchester wanaelekeza nguvu zao kwa kipa Dean Henderson wa Sheffield United endapo de Gea ataamua kuondoka.

Hayo yakijiri, kocha Pep Guardiola wa Manchester City amesema yeyote kati ya Fernandinho na Kyle Walker anaweza kuziba pengo la beki Atmaric Laporte aliyeumia majuzi.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa alitolewa kwa msaada wa machela wakati wa mechi hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ambapo Man-City waliishinda kwa 4-0.

Kuumia kwa Laporte kumekuja muda wa siku chache tu baada ya Guardiola kumtaja kama beki wake mkali zaidi kikosini kwa sasa, lakini haijulikani atakuwa nje kwa muda gani.

You can share this post!

Rais Kenyatta atarajiwa kufungua rasmi maonyesho ya...

AFC yawakia Gor kuhusu usajili wa Makwatta

adminleo