• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 10:55 AM
Sikuwa na uhakika kwamba Auba angerefusha muda wake Arsenal – Arteta

Sikuwa na uhakika kwamba Auba angerefusha muda wake Arsenal – Arteta

Na MASHIRIKA

KOCHA Mikel Arteta wa Arsenal amefichua kwamba alikuwa na shaka tele iwapo nahodha na mvamizi Pierre-Emerick Aubameyang angetia saini mkataba mpya uwanjani Arsenal tangu alipopokezwa mikoba ya kikosi hicho mnamo Disemba 2019.

Hata hivyo, Aubameyang, 31, alirefusha kipindi cha kuhudumu kwake kambini mwa The Gunners mnamo Septemba 15, 2020 kwa miaka mitatu zaidi hadi mwishoni mwa 2023.

Kwa mujibu wa maelewano hayo mapya, Arsenal sasa watakuwa wakimlipa Aubameyang ujira wa hadi Sh35 milioni kwa wiki.

Mkataba wa awali kati ya nyota huyo raia wa Gabon na Arsenal ulitarajiwa kukatika rasmi mnamo Juni 2021. Hadi kufikia sasa, fowadi huyo wa zamani wa Borussia Dortmund amefungia Arsenal jumla ya mabao 72 kutokana na mechi 111.

Alikuwa sehemu muhimu katika ushindi wa Kombe la FA mnamo 2019-20 dhidi ya Chelsea na akasaidia waajiri wake kubwaga Liverpool kwenye Community Shield mwanzoni mwa msimu huu wa 2020-21.

“Nilipojiunga na Arsenal, nilikuwa na shaka kubwa. Mwanzo ni kwa sababu kikosi hakikuwa na fedha ya kukisuka upya kikosi kwa kuleta wanasoka ambao ushirikiano nao na Aubameyang ungemwaminisha kusalia Emirates,” akatanguliza.

“Nadhani Aubameyang pia alikuwa na shaka kuhusu mambo mengi. Ingekuwa rahisi sana kwake kufanya maamuzi ya kuondoka kwa sababu alikuwa akiwaniwa na miamba kama vila Real Madrid, Juventus, Inter Milan, Barcelona na Chelsea.”

“Hata hivyo, nilimsihi avute subira na kwa kweli, maombi yalijibiwa na uvumilivu ukatuletea mambo mabivu,” akasema sogora huyo wa zamani wa Everton na Arsenal.

Aubameyang alijiunga na Arsenal mnamo Januari 2018 baada ya kuagana na Dortmund ya Ujerumani kwa kima cha Sh7.8 bilioni.

Katika msimu wake wa kwanza mkamilifu kwenye soka ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo 2018-19, alipachika wavuni jumla ya mabao 23 na akatawazwa mfungaji bora kwa pamoja na Sadio Mane na Mohamed Salah wa Liverpool.

“Ilikuwa vyema na muhimu zaidi kwa Aubameyang kusalia nasi ugani Emirates. Ni mchezaji wa haiba kubwa aliye na uwezo mkubwa ndani na nje ya uwanja,” akasema Arteta.

“Aubameyang ni kiongozi muhimu kwa Arsenal na sehemu kubwa ya mpango wetu wa kujisuka upya. Anatamani kuwa huko juu pamoja na wanasoka wengine wa haiba kubwa duniani ilia ache taathira za kudumu katika ulingo wa soka,” akaongeza Arteta.

Katika mechi 86 za EPL, amepachika wavuni mabao 55 na kuchangia mengine 12. Amewahi pia kuvalia jezi za AC Milan, Dijon, Lille, Nice, AS Monaco, Bastia, Dijon na Saint-Etienne.

Mshindi huyo wa taji la Mwanasoka Bora wa Mwaka 2015 barani Afrika alipokezwa utepe wa unahodha wa Arsenal mnamo Novemba 2019 baada ya mtangulizi wa Arteta, kocha Unai Emery kumvua kiungo Granit Xhaka unahodha wa kikosi.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Man-United pua na mdomo kumsajili beki Alex Telles

Leicester kujinasia fowadi matata wa Uturuki, Cengiz Under...