Michezo

Wanaraga wa Simbas kuraruana na Milki za Kiarabu kabla ya Kombe la Afrika

Na GEOFFREY ANENE May 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KENYA Simbas wamepata mechi ya kupimana nguvu dhidi ya Milki za Kiarabu kabla ya Kombe la Afrika la raga ya wachezaji 15 kila upande mwezi ujao wa Juni.

Vijana wa kocha Jerome Paarwater watakabana koo na Milki za Kiarabu hapo Mei 24 ugani RFUEA mjini Nairobi kabla ya kuelekea Afrika Kusini kwa kambi ya mwezi mmoja.

Simbas walirarua Milki za Kiarabu 55-12 mara ya kwanza na mwisho walikutana mnamo Desemba 16, 2011 mjini Dubai katika shindano la mataifa manne la Cup of Nations lililohusisha pia Brazil na Hong Kong.

Vijana wa Paarwater wako kambini wakati huu mjini Kakamega kwa dimba hilo la Afrika ambalo pia mshindi atajikatia tiketi kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2027. Milki za Kiarabu nao wanajiandaa kwa Kombe la Bara Asia litakalofanyika baadaye mwaka huu.

Paarwater, ambaye ni raia wa Afrika Kusini, ana wachezaji 50. “Wachezaji 33 kutoka orodha hii watakusanyika Mei 26 kwa kambi ndogo kabla ya kuelekea Afrika Kusini mnamo Mei 28 kwa kambi mbili za hali ya juu,” akasema Paarwater.

Kambi ya kwanza nchini Afrika Kusini itakuwa Mei 28 hadi Juni 22 mjini Cape Town kwa ushirikiano na timu ya Western Province. Mjini Cape Town, Simbas itashiriki mechi dhidi ya timu kutoka ligi ya Currie Cup kila Jumamosi halafu mazoezi ya kugongana dhidi ya klabu za mtaani na zile za vyuo vikuu.

Awamu ya pili itashuhudia Simbas wakihamia mjini Nylstroom kushirikiana na Blue Bulls mnamo Juni 22-27. Kambi hii ya pili itashuhudia Simbas wakivaana na vikosi vya Blue Bulls vya Currie Cup siku ya Jumanne na Alhamisi,” akaongeza.

Mechi kati ya Simbas na Milki za Kiarabu itasakatwa kuanzia saa tisa alasiri. Kiingilio ni Sh500 (tiketi za kawaida) na Sh1,000 (tiketi za watu mashuhuri).

Tiketi zinauzwa kupitia tovuti ya www.tikohub.com.