Simbas na Lionesses zatua Uganda kutafuta ufanisi Elgon Cup
Na GEOFFREY ANENE
TIMU za Kenya za raga ya wachezaji 15 kila upande Simbas (wanaume) na Lionesses (wanawake) ziko jijini Kampala tayari kwa mechi za marudiano za Kombe la Elgon dhidi ya Uganda zitakazosakatwa uwanjani Kyadondo mnamo Julai 13, 2019.
Simbas, ambayo iko chini ya kocha Albertus Van Buuren baada ya Paul Odera kuandamana na ile ya chipukizi nchini Brazil, itakuwa ikilenga kufuta kichapo cha alama 16-13 ilichopata uwanjani Mamboleo mjini Kisumu katika mechi ya mkondo wa kwanza Juni 22.
Lionesses ina kazi rahisi ya kutwaa taji baada ya kuzamisha She-Cranes ya Uganda 42-13 Juni 22.
Ilivuna ushindi huu mkubwa kupitia kwa nahodha Philadelphia Olando (miguso mitatu), Grace Adhiambo (mguso, mkwaju), Celestine Osinde (mguso), Janet Okello (mguso), Sophia Ayieta (mguso) na Stella Wafula (mguso).
Uganda ilijiliwaza na alama kutoka kwa Shalot Mudola (penalti na mguso) na Winnie Atiang (mguso).
Katika mechi ya mkondo wa kwanza, Simbas ilijipata chini alama 0-11 baada ya Adrian Kasito kufunga mguso bila mkwaju. Aaron Ofoyrwoth aliimarisha uongozi wa Waganda kupita bao la alama tatu (drop goal) kabla ya kufanya mambo kuwa 11-0 alipopachika penalti.
Dominic Coulson, ambaye anaongoza kampeni ya Chipu nchini Brazil, alipunguza mwanya huo hadi 11-3 kupitia kwa penalti, lakini Uganda ilijibu kupitia mguso kutoka kwa Santos Senteza 16-3.
Kugonga mlingoti
Kenya ilipata mguso wake wa kwanza na kufanya mambo kuwa 16-8 kupitia kwa Griffin Musila, lakini mkwaju wa Coulson uligonga mlingoti na kutoka nje.
Mguso mwingine kutoka kwa Geoffrey Okwach ulileta Kenya karibu na Uganda 16-13, huku mkwaju ukijaa nje.
Ofoyrwoth aliibuka mchezaji bora wa mechi.
Matokeo ya mechi ya kwanza yanaweka Simbas pabaya kupoteza taji ambalo imeshinda tangu mwaka 2016.