• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Simbas waenda kuwinda Victoria Cup

Simbas waenda kuwinda Victoria Cup

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Kenya cha Raga ya wachezaji 15 kila upande almaarufu Simbas kiliondoka humu nchini hapo jana kuelekea Zambia kuwania ubingwa wa Victoria Cup 2019.

Kenya watafungua kampeni zao katika kipute hicho dhidi ya wenyeji Zambia mnamo Jumamosi kisha kuchuana na Zimbabwe mnamo Agosti 3.

Simbas wanashiriki kivumbi hicho wiki mbili baada ya kuwazamisha Uganda na kutia kapuni ufalme wa Elgon Cup.

Katika mapambano hayo ya Victoria Cup, kocha Paul Odera amefichua azma ya kudumisha kikosi chake kilichotamalaki mashindano ya mikondo miwili ya Elgon Cup.

Kikosi cha Kenya kitakuwa chini ya nahodha Jacob Ojee ambaye alitawazwa mchezaji bora wa kivumbi cha Elgon Cup baada ya kuwavunia Simbas pointi 11 kati ya 16

Baada ya kukamilisha mechi za mkondo wa kwanza, Kenya watarudiana na Zambia mnamo Agosti 21 kisha Zimbabwe mnamo Agosti 24 jijini Nairobi.

Kufufuliwa kwa Victoria Cup kunachochewa na hatua ya kufutiliwa mbali kwa kivumbi cha Rugby Africa Gold Cup kutokana na ukosefu wa udhamini.

Wapinzani

Vikosi vingine ambavyo vimepangwa katika kundi moja na Kenya katika kinyang’anyiro hicho ni Uganda na Zambia.

Simbas walinyanyua ubingwa wa taji la Elgon Cup kwa jumla ya alama 29-21 hasa ikizingatiwa kwamba Uganda waliwapepeta 16-13 katika mchuano wa mkondo wa kwanza uliowakutanisha jijini Kisumu.

Kulingana na Thomas Odundo ambaye ni mkurugenzi wa Shirikisho la Raga la Kenya (KRU), kiini cha kutatizwa kwa Simbas katika kivumbi hicho ni mengi ya mabadiliko ambayo kikosi hicho kilifanyiwa.

Licha ya kuokota alama 1.2 pekee baada ya ushindi huo dhidi ya Uganda, Simbas wanasalia katika nafasi ya 32 duniani huku pengo dogo la chini ya alama moja likitamalaki kati yao na Korea waliopo juu yao.

  • Tags

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Nilikawia kumwambia nampenda, sasa...

AKILIMALI: Maembe yana mapato kwa wanaokuza miche...

adminleo