• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 10:50 AM
Smalling atia saini mkataba wa miaka mitatu AS Roma

Smalling atia saini mkataba wa miaka mitatu AS Roma

Na MASHIRIKA

AS Roma wamemsajili beki wa Manchester United, Chris Smalling kwa mkataba wa miaka mitatu uliorasimishwa kwa kiasi cha Sh1.9 bilioni.

Hata hivyo, ada hiyo huenda ikaongezeka hadi Sh2.5 bilioni.

Usajili huo wa Smalling ulikamilishwa na Shirikisho la Soka la Italia dakika moja kabla ya muhula wa uhamisho wa wachezaji kufungwa rasmi mnamo Oktoba 5, 2020.

Smalling, 30, aliwajibikia Roma kwa mkopo msimu uliopita na akasaidia kikosi hicho cha kocha Paulo Fonseca kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Italia (Serie A) katika nafasi ya tano na hivyo kufuzu kwa kipute cha Europa League.

Iliwachukua Man-United na Roma muda mrefu kuafikiana kuhusu uhamisho wa Smalling aliyesema: “Hakuna jambo zuri maishani ambalo hutokea kirahisi. Mawazo na moyo wangu wote umekuwa Roma. Nina furaha tele kusalia kambini mwa kikosi hiki ambacho kimenipa jukwaa zuri la kujifufua kitaaluma.”

Kwa kipindi cha mwaka mmoja kambini mwa Roma, Smalling aliwajibishwa mara 30 na akafungia kikosi hicho mabao matatu mnamo 2019-20.

Nyota huyo amechezea Uingereza mara 31 na aliwahi kuwajibishwa na Man-United mara 323 ambapo aliwasaidia mataji mawili ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Kombe la FA mara moja, taji moja la League Cup na ufalme wa Europa League mara moja.

Kabla ya kutangaza rasmi kuondoka kwa Smalling, Man-United walikamilisha usajili wa beki wa kushoto raia wa Brazil, Alex Telles kwa mkataba wa miaka minne kutoka FC Porto.

Man-United walisajili pia fowadi mkongwe Edinson Cavani na chipukizi Amad Diallo kutoka Atalanta katika siku ya mwisho ya uhamisho wa wachezaji muhula huu.

You can share this post!

Serikali ‘yachapisha’ pesa mpya kufufua uchumi

BURUDANI: Alfa Ryus alianza kwa kuiga, sasa ni mwanamuziki...