Michezo

SOKA MASHINANI: Mang'u Stars FC

August 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

MANG’U Stars FC ni ndimu ambayo imeanza kupata umaarufu na uungwaji mkono katika eneo la Gatundu Kaskazini, Kaunti ya Kiambu.

Chini ya kocha wake Francis Ngige, timu hii imepiga hatua kubwa kispoti licha ya kukumbwa na changamoto nyingi.

“Nitafanya juhudi kuona ya kwamba nimeweka timu hii imara licha ya shida nyingi,” akasema Ngige wakati akihojiwa na safu ya michezo.

Katika msimu huu wa 2019 timu hiyo ilishiriki Aberdare Regional League ambapo ilianza katika Kundi B ma kukamilisha Ligi hiyo kwenye nafasi ya sita na alama 25.

Kocha huyo anasema baada ya kukamilisha Ligi hiyo, kwa wakati huu wanajishirikisha na mechi za kirafiki, huku wakipata matokeo ya kuridhisha.

Katika mechi ya hivi majuzi vijana hao wa Mang’u Stars waliitesa Kamwangi Youth kwa bao 1-0.

Chipukizi hao wepesi walitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Chania Raiders.

Kocha Ngige anasema licha ya timu hiyo kubuniwa zaidi ya miaka 12 zilizopita, imekuwa ikiyumbishwa na changamoto tele.

Timu yahitaji vifaa muhimu

“Kwa wakati huu timu hiyo yenye wachezaji 28 inahitaji vifaa muhimu vya kuchezea vikiwemo jezi, na viatu. Tumejaribu tuwezavyo kutafuta ufadhili lakini wadau bado hawajachukua jukumu hilo kisawasawa,” alisema kocha huyo.

Timu hiyo inajivunia kuwa na wachezaji mahiri wenye ujuzi tele, ambao wameonyesha nidhamu ya hali ya juu; ambacho ndicho kigezo cha kufanikisha ufanisi wa mchezaji yeyote yule.

Kikosi kamili kinachokipa timu hiyo uhai ni magolikipa Edward Ngige, na Simon Maina.

Katika difensi kuna majabali kama Joseph Muturi, Martin Gaichunga, Paul Muiruri, na Joseph Muturi.

Kiungo kuna Joseph Njoroge, Jeremiah Maina, Issc Ndung’u, na Kevin Ng’ang’a.

Mastraika ni Joseph Mungai, Simon Kamau, na Francis Muturi.

Kocha huyo ana imani kuwa timu hiyo itajipanga vyema msimu ujao kwa sababu wana mashabiki sugu ambao wameahidi ‘kufanya jambo’ ifikapo msimu ujao.

Akiongea na Taifa Leo, nahodha wa timu hiyo, Martin Gachunga, alisema timu hiyo ina mipango mikubwa kwani inatarajia kuwa na timu ya vijana chipukizi ili kuipa nguvu timu hiyo.

Wao hufanya mazoezi katika uwanja wa shule ya msingi ya Mang’u Primary baina ya Jumanne na Ijumaa kila wiki.