Son adai mazoezi ya jeshi yalimsaidia kupona
Na CHRIS ADUNGO
FOWADI Son Heung-min wa Tottenham Hotspur amekiri kwamba japo zoezi la huduma za kijeshi alilolishiriki hivi majuzi nchini mwao Korea Kusini lilikuwa “gumu kupindukia”, lilimsaidia sana kurejea katika fomu nzuri kadri anavyojiandaa kwa marejeo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Son, 27, alishiriki huduma za kijeshi nchini Korea kwa kipindi cha wiki tatu mnamo Aprili baada ya kupona jeraha lililomshuhudia akifanyiwa upasuaji wa mkono.
“Kilikuwa kipindi kigumu cha wiki tatu. Hata hivyo, nilipata fursa maridhawa ya kurejelea katika hali nzuri ya fomu. Japo siwezi kufichua kila kitu nilichofanya, nathibitisha kwamba nilifurahia zoezi zima,” akatanguliza.
“Siku za mwanzo zilikuwa ngumu zaidi kwa kuwa hatukuwa tunafahamiana vyema. Tuliishi watu 10 kila siku katika chumba kimoja. Baada ya kujuana na kuzoeana, zoezi lilianza kuvutia, ushirikiano ukawa wa kiwango cha juu na urafiki ukakithiri,” akaongeza Son.
Son alipata jeraha la mkono katikati ya Februari 2020, mwezi mmoja kabla ya kivumbi cha EPL kusitishwa kwa muda kutokana na janga la corona.
Awali, kocha Jose Mourinho alikuwa akihofia kwamba Son na mvamizi mwenzake Harry Kane wasingenogesha mchuano wowote msimu huu. Ilivyo, wawili hao watakuwa sasa tegemeo kubwa la Tottenham ambao wanalenga kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.
Zikisalia mechi tisa zaidi kwa kampeni za muhula huu kutamatika rasmi, Tottenham kwa sasa wana alama saba zaidi nyuma ya Chelsea ambao wanafunga mduara wa nne-bora.
“Nahisi kwamba nimepona kabisa, hasa baada ya kuhudumu katika jeshi la Korea Kusini kwa majuma matatu. Nimekuwa pia nikishiriki mazoezi ya pamoja na Moussa Sissoko, Kane na Steven Bergwijn kwa kipindi cha wiki mbili zilizopita,” akasema Son.