Michezo

South B United imani tosha taji la Chapa Dimba ni lao

May 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya South B United imepania kutwaa ubingwa wa taji la Chapa Dimba na Safaricom Seasom Two.

Kocha wake anasema John Mandela anasema kwamba ana imani tosha vijana wake watatimiza azimio hilo kwenye fainali za kitaifa zitakazochezewa Kinoru Stadium Kaunti ya Meru Mwezi Juni mwaka huu.

Kocha huyo anadai wamepania kumalizia shughuli pale zilipoachiwa na Gor Mahia Youth katika fainali za msimu uliyopita.

”Tunaendelea na mazoezi yetu kujiweka vizuri kukabili washiriki wengi katika fainali za kitaifa maana wote wanalenga taji hilo la pekee lakini kamwe hatuweza kuwadharau,” alisema na kuongeza kwamba wataenda kushindana wala siyo kulaza damu katika mji wa Meru.

Kocha huyo anashukuru kikosi chake kwa kazi nzuri kilichofanya na kufuzu kwa fainali za kitaifa baada ya kubanduliwa na Gor Mahia Youth kwenye nusu fainali ya kipute hicho msimu uliyopita.

Kadhalika anatoa pongezi tele kwa Enock Wanyama wa kikosi hicho aliyetuliwa katika kikosi cha taifa kinachotarajiwa kwenda nchini Uhispania kushiriki mazoezi ya mchezo huo.

South B United iliibuka mabingwa wa kipute hicho Mkoa wa Nairobi ilipovuna ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Jericho Allstars katika fainali iliyochezewa Uwanjani Goan Institute Pangani Nairobi.

Kwenue nusu fainali South B United ilinasa tiketi ya fainali ilipokomoa Uweza FC kwa mabao 2-0 nayo Jericho Allstars ilivuna ufanisi wa mabao 2-1 dhidi ya Brightstar Academy.

Kadhalika South B United ilifuzu kushiriki fainali za Mkoa wa Nairobi baada ya kunyamazisha Vapor Sports kwa mabao 5-4 kupitia mipigo ya matuta kwenye fainali za FKF Tawi la Nairobi West.

South B United inajumuisha wachezaji kama: Kaysha Kerenre, Achweya Cedrine, Erick Balecho, Karani Clifford, Boniface Mwirigi, Meshack Omondi, Wilson Anguli, Enock Wanyama, Kepha Wanjala, Alvin Kuka, Victor Madegwa, Mohammed Abdi Razak, Mohammed Suleiman, Mohammed Hussein, Brian Ngolo, Brian Munene, Rex Ochieng na Ogolla George bila kumsahau meneja wake Masese Moki.

Mabingwa hao wamejiunga na wenzao kutoka Mikoa mingine ikiwamo: Super Solico Boys-wavulana na St Marys Ndovea-wasichana (Mashariki) Al Ahly na Kitale Queens wavulana na wasichana(Rift Valley), Lugari Blue Saints (wavulana) na Bishop Njenga Girls (Magharibi), Manyatta Boys na Ndhiwa Queens(Nyanza), Shimanzi Youth-wavulana na Changamwe Ladies(Mombasa), wavulana wa Berlin (Kaskazini Mashariki), Euronuts Boys na Barcelona Ladies (Mkoa wa Kati) na Acakoro Ladies (Mkoa wa Nairobi).